;Wakala wa Vipimo (WMA) Tanzania imeendelea na zoezi la utoaji wa elimu pamoja na uhakiki wa mizani kwenye makampuni mbalimbali ya wafanyabiashara Mkoani Mwanza katika Wilaya za Kwimba, Magu, Misungwi na Sengerema ikiwa ni maandalizi ya msimu wa Pamba.
Akizungumza na Meneja wa Wakala wa Vipimo Mkoani Mwanza Bwana Hemed Kipengele alisema jumla ya mizani 448 tayari imekaguliwa kutokana na makampuni manne ambayo tayari yamekagulisha mizani yake na imekutwa ikiwa sahihi ambayo ni ICK (T) LTD ambao walikuwa a mizani 184, SM HOLDING wenye jumla ya mizani 85 pamoja na NYANZA COTTON ambao walikuwa na mizani 179. Meneje aliongezea kuwa zoezi hili la utoaji elimu pamoja na uhakiki wa mizani itakayotumika kununulia Pamba linaendelea kwa Mikoa yote inayolima Pamba ambayo ni Shinyanga, Simiyu, Geita, Kagera, Tabora pamoja na Mara.
Bwana Kipengele alisema wanatarajia kutembelea jumla ya vijiji 101 ambavyo vina jumla ya vituo vya kuuzia Pamba 150 ili waweze kutoa elimu na kufanya kaguzi za kushutukize kwa wanunuzi wa Pamba ili kuona kama mizani waliyopima na ikaonekana ni sahihi itaendelea kununua Pamba ya wakulima kwa vipimo sahihi.
Meneja Kipengele aliwasihi baadhi ya wakulima wanaolalamikiwa kuweka maji, kokoto pamoja na mchanga kwenye Pamba kwa ajili ya kuongeza uzito waache tabia hiyo mara moja sababu Sheria ya vipimo ipo na inafanyakazi kwa pande zote mbili muuzaji na mnunuzi wote kwa pamoja hawatakiwi kufanya udanganyifu wowote katika biashara.
Kipengele alisema Sheria ya Vipimo Sura 340 inawataka Wakala wa Vipimo kuhakiki na kupiga chapa vipimo vyote vinavyotumika katika biashara pia Wakala wa Vipimo imeongeza na uwekaji wa sticker kwa kipimo kitakachokuwa tayari kimehakikiwa ili iwe rahisi kwa wakulima kuona na kutambua mizani iliyokaguliwa na kuruhusiwa kwa biashara kwa mwaka husika.
Alisisitiza kuwa kwa wale watakaobainika kuchezea mizani kwa ajili ya kuwaibia wakulima adhabu ni kuanzia laki moja hadi milioni ishirini endapo mkosaji atakubali kosa, endapo kesi itafikishwa mahakamani na mlalamikiwa akakutwa kweli alikosa kulingana na ushahidi utakaokuwa umetolewa mshitakiwa atatozwa faini kuanzia laki tatu hadi milioni hamsini au kifungo cha miaka mitatu au vyote kwa pamoja. Lengo kuu ni kumlinda mlaji ili apate faida na thamani ya kile alichozalisha na siyo kupunjwa na wafanyabiashara wajanjawajanja.
Tunaimani Tanzania ya viwanda itafanikiwa endapo Mkulima, Mfanyabiashara watazingatia matumizi ya vipimo sahihi kuanzia maandalizi ya shamba, upandaji wa mazao, utumiaji wa pembejeo, uuzaji, usafarishaji, upokeaji wa mazao, ufungashaji hadi utumiaji wa mazao yenyewe , hivyo vyote vikizingatia matumizi ya vipimo sahihi viwanda vingi vitaweza kupata malighafi za kutosha sababu mkulima na mfanyabiashara kila mtu atakuwa na imani na mwenzake kupitia matumizi ya vipimo sahihi. Msema kweli na mleta haki katika biashara ni kipimo sahihi kilichohakikiwa na Wakala wa Vipimo wala siyo vinginevyo.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.