Serikali ya mkoani hapa imesema mkoa wa Mwanza bado unakabiliwa na tatizo la Utapiamlo unaotokana na lishe duni pamoja na lishe iliyozidi inayosababishwa na watu kutozingatia maelekezo ya wataalamu.
Akifungua kikao cha wadau wa lishe mkoani hapa, Katibu Tawala mkoa wa Mwanza aliyewakilishwa na Bwana Johaness Bukwali ambae ni Katibu Tawala Msaidizi huduma za Uchumi na uzalishaji, alisema takwimu zinaonesha kuwa viwango vya watoto chini ya miaka mitano waliodumaa kwa mwaka 2015/2016 ni asilimia 39.
Bukwali alisema watoto wenye ukondefu ni asilimia 4.3 na walio na uzito pungufu ni asilimia 14.1.
Bukwali alisema kuwa kwa upande wa upungufu wa damu ni asilimia 27 kwa watoto walio chini ya umri wa miaka mitano,upande wa kundi la wakina mama wenye uwezo wa kuzaa yaani umri kati ya miaka 15 hadi 49 zaidi ya asilimia 45 wanaupungufu wa damu na hukumbwa na matatizo wakati wa kujifungua.
Kwa upande wake Kaimu mkurugenzi mtendaji wa taasisi chakula na lishe Tanzania Dkt. Joyceline Kaganda, amesema tatizo kubwa linaloikabili jamii ni uelewa duni wa masuala ya lishe na umuhimu wake.
“Unakuta wakina mama anatakiwa kwenda klliniki mara kwa mara lakini haendi mpaka ujauzito ufikishe miezi nane ndipo ananza kwenda na kupewa elimu ya lishe.” alisema Dkt. Kaganda.
Kwa upande wake afisa wa lishe kutoka mkoani hapa, Sophia Lugome amesema kutokana na kubadilika kwa mfumo wa maisha imechangia ongezeko la lishe duni kwakuwa mzazi wa kike ambaye hapo awali alikuwa na jukumu kubwa la malezi kwa watoto hivi sasa hali ni kiunyume, unakuta wazazi wote mpo kwenye majukumu na hivyo malezi yamebakia kuwa jukumu la wajakazi, ambao kimalezi katika suala la lishe tunashauri watoto wale mara kwa mara, suala ambalo kwa mjakazi kwake inaweza isiwe hivyo katika kumuhudumia mtoto.
Meneja mradi msaidizi kutoka (Global Alliance for Improvement Nutrition) Julius Saimon amesema uelewa kwa makundi ya baadhi ya watu umeanza kuongezeka tofauti na ilivyokuwa hapo awali.
“kundi la wafanyabiashara ni moja ya kundi ambalo muitikio wao ni mkubwa ukilinganisha na hapo awali” amesema Julius
Kwa upande wake Kaimu Mganga Mkuu wa mkoani hapa Dkt. Silas Wambura, amesema mkoa wa Mwanza ambao unakadiriwa kuwa na watu Mil. 3 kwa sasa hauwezi kubaki nyuma katika suala zima la lishe kwani ili maendeleo yaweze kufikiwa, kitu kikubwa ni rasilimali watu.
“Tunapoelekea kwenye Uchumi wa kati na Tanzania ya Viwanda katika mpango wa miaka mitano ijayo, nguvu kazi ni muhimu sana na ili tuwe na nguvu kazi imara suala la afya lazima tulipe kipaumbele, hivyo semina hii inayo wakutanisha wadau wa lishe ni muhimu sana kwa sasa.” amesema Wambura.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.