Mkoa wa Mwanza umeanza rasmi utekelezaji wa awamu ya kwanza ya usajili na ugawaji wa kadi za Bima ya Afya kwa Wote, ambapo jumla ya kaya 19,344 zenye wanufaika 85,265 zitasajiliwa. Uzinduzi huo umefanywa na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhe. Said Mtanda, aliyesisitiza umuhimu wa bima katika kukabiliana na gharama za matibabu zisizotarajiwa.

Mhe. Mtanda amesema hakuna anayepanga kuugua, hivyo bima ya afya ni kinga muhimu ya kifedha kwa familia. Ameeleza kuwa gharama za matibabu mara nyingi ni kubwa na zinaweza kuathiri mipango ya maendeleo ya kaya, hivyo mpango huo ni mkombozi kwa wananchi.

Katika utekelezaji wa zoezi hilo, timu za usajili zitafika katika kila kijiji na mtaa, kata na halmashauri zote za mkoa huo. Amesema majina ya wanufaika wa awamu ya kwanza tayari yameainishwa na kusambazwa hadi ngazi ya vijiji na mitaa, na zoezi limeanza rasmi.

RC Mtanda amewataka walengwa kuhakikisha wanajitokeza kwa wakati kusajiliwa. Ameonya kuwa atakayeshindwa kujitokeza bila sababu halali atapoteza fursa hiyo na atalazimika kujilipia mwenyewe baadaye.

Aidha, ametangaza kuwa usajili kwa wanufaika watakaolipia bima kwa gharama zao utaanza hivi karibuni, na taarifa rasmi itatolewa kupitia vyombo vya mawasiliano vya Serikali.

Akizungumza katika hafla hiyo, Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Dkt. Gabriel Mashauri amesema uzinduzi huo ni utekelezaji wa maono ya Rais wa Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha wananchi wanapata matibabu ya uhakika.

Dkt. Gabriel pia amempongeza RC Mtanda kwa kuwa balozi mzuri wa uhamasishaji wa bima ya afya, akisema amekuwa akitumia kila jukwaa kuelimisha na kuhamasisha wananchi kujiunga na mpango huo pindi dirisha la usajili linapofunguliwa.

Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.