Mradi wa Kizazi Hodari watambulishwa Mwanza
Serikali kupitia OR- TAMISEMI kwa kushirikiana na Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Makao Makuu Arusha, limetambulisha mradi wa USAID Kizazi Hodari Mkoani Mwanza ambao umelenga kuwafikia watoto 64,266.
Akizungumza jijini Mwanza leo wakati akitambulisha mradi huo Kiongozi wa Mradi wa USAID Kizazi Hodari Kanda ya Kaskazini Mashariki, KKKT Makao Makuu Arusha, Dk. Godson Maro, amesema lengo kubwa la mradi huo ni kuboresha afya,ustawi na ulinzi kwa watoto walio katika mazingira hatarishi na vijana walio katika maeneo ambayo yana maambukizi ya juu ya virusi vya ukimwi.
Dk.Maro amesema kwamba wanatekeleza mradi huo wa miaka mitano ulioanza Aprili Mosi ,2022 Mkoani Arusha na Kilimanjaro kwa ufadhili wa Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa(USAID) ambao utagharimu dola milioni 27.4 unaotarajia kukamilika Machi 31, 2027 ukiwa umewafikia walengwa katika mikoa mingine sita ambayo ni Dodoma,Singida, Manyara, Geita, Mara na Mwanza.
“Katika Mkoa wa Mwanza mradi huu umelenga kuwafikia watoto 64,266 wanaoishi katika mazingira hatarishi ambao wameathirika au kuathiriwa na virusi vya ukimwi kwa ajili ya kuwaunganisha na huduma za tiba ambazo zitawasaidia kufubaza virusi vya ukimwi, tunawapa elimu ya kujitambua pamoja na huduma zingine jumuishi,”amesema Dk. Maro na kuongeza
“Walengwa wa mradi huu ni watoto wenye umri wa miaka 0 hadi miaka 17, pia tutatambua kaya maskini zenye uhitaji na kuziunganisha kwenye vikundi mbalimbali vya maendeleo ili viwasaidie kuongeza kipato cha kaya waweze kuwahudumia watoto wenye.
maambukizi,”amefafanua
Afisa Ustawi wa Jamii kutoka OR-TAMISEMI Mariam Nkumbwa, ametoa rai kwa watu wote watakaohusika katika kutekeleza mradi huo kuwajibika na kufanya kazi kwa kushirikiana ili malengo ya mradi huo yatimie kwa ufasaha.
“Matarajio ya OR- Tamisemi kwenye mradi huu ni kuona matokeo yote chanya yaliyoainishwa yanatekelezwa kama kutekelezwa kama yalivyopangwa, tunaamini wakati wa utekelezaji wa miradi huwa kuna changamoto mbalimbali zinajitokeza, tunaouzoefu kupitia miradi mbalimbali tuliyokwishaitekeleza lakini tukifanya kazi kama timu tutashirikiana ili kuzitatua,”amesisitiza.
Awali akizungumza na wadau wanaotekeleza mradi huo ofisini kwake, Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza, Balandya Elikana alisema uongozi wa mkoa huo utashirikiana nao kuhakikisha kuwa malengo ya mradi yanafikiwa.
Afisa Ustawi wa Jamii Mkoa wa Mwanza, Faithmary Lukindo amesema mradi huo utasaidia watoto wenye maambukizi ya Virusi vya Ukimwi kutokushindwa kwenda shuleni kutokana na kusumbuliwa na magonjwa nyemelezi kwa sababu watakuwa na afya nzuri kutokana na kufuata ufuasi mzuri wa dawa pia watawasaidia kupatikana kwa vifaa saidizi pamoja na vifaa vya shuleni ili wasikose masomo.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.