Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda ametoa agizo kwa Mganga Mkuu wa Mkoa kuhakikisha Zahanati ya Nyambiti iliyopo Mtaa wa Nyambiti, katika Manispaa ya Ilemela inapatiwa Mtaalamu wa Maabara pamoja na vifaa muhimu ili kuwasaidia wananchi kupata huduma za uchunguzi wa afya karibu na makazi yao.

Mhe. Mtanda ametoa agizo hilo wakati wa ziara yake ya kikazi ya kukagua ujenzi wa Zahanati ya Nyambiti Kata ya Buzuruga, ambapo amesema kuwa hakuna sababu ya wananchi kusafiri umbali mrefu kwenda Hospitali za Rufaa, Mkoa au Wilaya ilhali huduma hizo zinaweza kutolewa katika zahanati hiyo.

Amesisitiza kuwa lengo la Serikali ni kusogeza huduma za afya karibu na wananchi ili kupunguza msongamano katika hospitali kubwa na kuhakikisha matatizo madogo ya kiafya yanatatuliwa katika ngazi ya chini.

“Tunajenga zahanati na vituo vya afya ili matatizo madogo madogo yamalizwe huko huko, badala ya kulundikana katika hospitali kubwa,” amesema Mhe. Mtanda.

Mkuu wa Mkoa amewahakikishia wananchi wa Nyambiti kuwa vifaa vya maabara vitapatikana baada ya maagizo aliyoyatoa kwa Mganga Mkuu wa Mkoa, huku akiahidi kufuatilia utekelezaji wa agizo hilo ndani ya kipindi cha miezi miwili.

Aidha, amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuidhinisha kiasi cha shilingi milioni 239 kupitia Sekta ya Afya kwa mwaka wa fedha 2024/2025, ambapo sehemu ya fedha hizo imetumika katika ujenzi wa Zahanati ya Nyambiti.

Katika hatua nyingine, Mhe. Mtanda amemuelekeza Mganga Mkuu wa Wilaya ya Ilemela kuhakikisha mfumo wa GOTHOMIS unafungwa ipasavyo ili kuwezesha baadhi ya changamoto za uendeshaji wa kituo hicho kutatuliwa kupitia mapato ya ndani.

Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.