RC MTANDA AAGIZA UKAGUZI MAALUM UJENZI WA JENGO LA WAZAZI HOSPITALI YA WILAYA UKEREWE
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda amemuagiza Katibu Tawala wa Mkoa huo kumpeleka Mkaguzi wa ndani wa Mkoa kukagua mwenendo wa utekelezaji wa ujenzi wa Jengo la wazazi katika Hospitali ya Wilaya ya Ukerewe kabla hajachukua hatua kwa wazembe watakaobainika.
Ametoa agizo hilo mapema leo ijumaa tarehe 27 Desemba, 2024 alipotembelea hospitalini hapo kukagua maendeleo ya ujenzi wa jengo la wazaz na kubaini kuna ucheleweshaji wa miezi 6 kinyume na mkataba na akaagiza ndani ya siku 20 likamilike.
“Serikali imeleta milioni 900 kwenye hospitali hii kwa ajili ya kujenga wodi muhimu ya wazazi ili kuboresha huduma bora za afya kwa wananchi na kuboresha hali ya utoaji huduma hivyo wasimamizi hampaswi kukwamisha juhudi hizi”. Mhe. Mtanda.
Ameongeza kuwa inashangaza kuona fedha zimeshafika tangu mwezi Machi mwaka huu na walipaswa kukamilisha ujenzi mwezi Juni lakini ni milioni 700 pekee zimelipwa kwa mafundi ikiwa ni asilimia 85 ya fedha zote na kusababisha kuchelewesha ujenzi huo.
Aidha, ameelekeza mzabuni wa milango kwenye hospitali hiyo ahakikishe anakabidhi mara moja ili iweze kuwekwa na kukamilisha ujenzi na kuhusu majengo yaliyotelekezwa yaliyoandaliwa kufanya upanuzi ameahidi kuwasiliana na wizara ili kuhakikisha fedha zinaletwa kukamilisha ujenzi.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.