Bakaa ya shilingi milioni 79 iliyosalia baada ya utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa miundombinu ya Hospitali ya Wilaya ya Ukerewe imeibua maswali kuhusu uwazi wa matumizi ya fedha za umma, hali iliyomlazimu Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhe. Said Mtanda, kuingilia kati na kuagiza ukaguzi wa haraka wa fedha hizo.

Akizungumza wakati wa ziara yake ya ukaguzi hospitalini hapo, Mhe. Mtanda amesema fedha hizo ni salio la mradi wa ujenzi wa hospitali, lakini hadi sasa hakuna mpango ulio wazi unaoeleza namna zilivyopangwa kutumika, jambo alilolitaja kuwa ni kinyume na misingi ya uwajibikaji na usimamizi wa fedha za Serikali.

Kutokana na hali hiyo, Mkuu wa Mkoa amemuelekeza Mkaguzi wa Ndani kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza kuwasilisha ripoti ya kina inayoeleza chanzo, mpango na matumizi yaliyopangwa ya fedha hizo ndani ya siku tatu.

“Ninajua fedha hizi zipo kama bakaa ya ujenzi wa hospitali, lakini matumizi yake hayajawekwa wazi kwa kiongozi yeyote. Haiwezekani kuendelea kuomba fedha mpya kutoka Serikalini ilhali fedha zilizopo bado hazina matumizi yanayoeleweka. Mkaguzi alete ripoti tujue ukweli,” amesisitiza.

Ameonya kuwa nidhamu na uwazi wa matumizi ya fedha za umma ni jambo lisilojadilika, akisisitiza kuwa viongozi wanapaswa kusimamia fedha kwa uadilifu ili kuleta matokeo chanya kwa wananchi.

Katika hatua nyingine, Mhe. Mtanda ameipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe kwa kutekeleza maelekezo aliyoyatoa awali, ikiwemo kukamilisha jengo la mama na mtoto pamoja na kufanya tathmini ya majengo ya hospitali ambayo hayajakamilika.

Amesema tathmini hiyo ni muhimu katika kuiwezesha halmashauri kuandaa maombi ya fedha za ukamilishaji kutoka Serikali Kuu ili kuhakikisha miundombinu ya hospitali inakamilika na kutoa huduma bora kwa wananchi.

Sambamba na hayo, Mkuu wa Mkoa amekagua mradi wa mtambo wa kuzalisha oksijeni katika hospitali hiyo na kuishukuru Serikali kwa kufanikisha utekelezaji wa mradi huo, akisema umeleta manufaa makubwa kwa wananchi wa Wilaya ya Ukerewe, hususan katika kuboresha huduma za afya.

Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.