RC MTANDA AIPONGEZA SENGEREMA DC KWA KUPATA HATI SAFI MIAKA 3 MFULULIZO
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda leo tarehe 17 Juni, 2025 ameshiriki kikao maalum cha Baraza la Madiwani kwa ajili ya kujadili hoja za Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) katika Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema na kuipongeza halmashauri hiyo kwa kupata hati safi ya ukaguzi.
Akizungumza katika kikao hicho, Mhe. Mtanda ameipongeza Halmashauri hiyo kwa kupata hati inayoridhisha kwa miaka mitatu mfululizo na namna ambavyo Halmashauri hiyo imepata hoja chache za ukaguzi.
Aidha, Mkuu wa Mkoa ameitaka Halmashauri hiyo kutekeleza maagizo na maelekezo ya Kamati ya Bunge ya Fedha za Serikali za Mitaa (LAAC) na hoja nne zilizobakia za ukaguzi sambamba na kulipa fedha zote zilizokopwa.
“Hakuna kuoneana aibu, hakuna kuonea huruma, lazima fedha za mikopo zilizokopeshwa zirudishwe, nataka niwahakikishieni lazima fedha zote zirudishwe dawa ya deni ni kulipa hakuna namna nyingine”. Mhe. Mtanda.
Kadhalika, Mhe. Mtanda ameitaka Halmashauri hiyo kuendelea kujibu hoja za CAG, na kuendelea kushirikiana na Ofisi hiyo kwa kuwa Halmashauri inaye Mkaguzi wa ndani hivyo amewataka kumtumia Mkaguzi huyo ili aisaidie Halmashauri kuweza kujifahamu hali zao kabla Mkaguzi wa nje hajafika.
Mbali na hayo, Mkuu wa Mkoa amesisitiza suala ubunifu amabapo ameitaka Halmashauri hiyo kuweka mikakati ya kubuni na kuanzisha miradi mikubwa ya kimkakati kwa kuwa Halmashauri ya Sengerema ni kubwa na haina mradi wowote wa kimkakati, ameshauri ubunifu huo uongezwe katika Baraza jipya litakaloundwa mara baada ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 2025.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.