RC MTANDA AWAPONGEZA JWTZ MWANZA KUTOA HUDUMA ZA AFYA BURE
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda amelipongeza Jeshi la wananchi wa Tanzania Mkoani humo kwa kuweka kambi ya matibabu bure ikiwa ni katika kuadhimisha miaka 60 ya jeshi hilo.
Pongezi hizo zimetolewa leo Agosti 28, 2024 mara baada ya kukagua mabanda ya kambi ya matibabu yaliyopo viwanja vya Furahisha Manispaa ya ilemela.
"Ninakupongeza Luteni kanali pamoja na wenzako kwa kuadhimisha miaka 60 ya jeshi kwa kutoa huduma za afya kwa wananchi wetu pamoja na kuendelea kuimarisha ulinzi ambalo ndio jukumu lenu". Amesema Mhe. Mtanda.
Aidha Mhe. Mtanda amewataka Wananchi kuendelee kushirikiana na serikali kwani serikali inaendelea kuboresha huduma za afya nchini na nia kubwa ni kutibu wananchi hivyo amewataka wananchi kufika kwenye hospitali ya jeshi pale Ilemela kwani kuna vifaa vya kisasa.
Sambamba na hayo pia Mhe. Mtanda amewatoa hofu wananchi wote wanaoendelea kuzuru katika viwanja hivyo kuwa watapatiwa huduma na hakuna yoyote kati yao atakayeachwa kwani Jeshi limemhakikishia hilo na kutoa rai pia kwa wananchi kuchangamkia fursa hiyo kwa kujitokeza kwa wingi.
Naye Luteni kanali Ahmedi Ali Shabhay amesema kama Hospitali ya Kanda ya Jeshi wamejipanga vyema kuhakikisha wanawahudumia wananchi wote watakaojitokeza, aidha amesema pia wamekua na ushirikiano kwa karibu na Wataalamu kutoka Damu salama na hivyo kupelekea kuwepo kwa huduma ya uchangiaji damu katika viwanja hivyo.
Aidha Luteni Kanali Shabhay ametumia wasaa huo pia kutoa wito kwa wananchi kufika katika hospitali ya jeshi ya kanda ya ziwa Magharibi iliyopo Mtaa wa Uwanja wa Ndege Wilayani Ilemela kwani wanatoa huduma mbalimbali za afya na amewakaribisha kufanyiwa uchunguzi na matibabu katika hospitali hiyo ambayo inahudumia wananchi wote.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.