Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda amewataka Maafisa Elimu wa Wilaya ya Ilemela kuanzia ngazi ya wilaya, kata hadi mitaa kuhakikisha wanakamilisha kwa asilimia 100 zoezi la uandikishaji wa wanafunzi wa darasa la awali, darasa la kwanza na kidato cha kwanza.

Agizo hilo amelitoa leo Februari 10, 2026 wakati wa ziara yake ya kukagua ujenzi wa maabara katika Shule ya Sekondari Buzuruga, ambapo amesema hali ya uandikishaji wa watoto katika Manispaa ya Ilemela bado hairidhishi ikilinganishwa na wilaya nyingine alizotembelea.

Mhe. Mtanda amesema baadhi ya wilaya tayari zimevuka lengo la uandikishaji na kufikia zaidi ya asilimia 95, hali iliyomfanya atoe wito kwa wazazi na walezi kutimiza wajibu wao kwa kuhakikisha watoto wote wenye sifa wanaandikishwa shule.

“Ninamuagiza Mkuu wa Wilaya kuhakikisha wazazi wote ambao hawajawapeleka watoto shule wanatafutwa popote walipo. Kwa kidato cha kwanza, hata mtoto asiye na viatu asikataliwe kuingia shuleni,” amesisitiza RC Mtanda.

Ameongeza kuwa walimu wanapaswa kushirikiana na wazazi wasio na uwezo wa kununua sare kwa kuingia makubaliano ya muda, ili kumpa nafasi mtoto kuendelea na masomo huku mzazi akitafuta namna ya kumfanisha na wenzake.

Katika hatua nyingine, Mkuu wa Mkoa amempongeza Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilemela, Bi. Ummy Wayayu, kwa kutenga shilingi milioni 60 kwa ajili ya ukamilishaji wa maabara za shule hiyo na kufanikisha upatikanaji wa shilingi milioni 30 hadi sasa.

“Ninakupongeza kwa jitihada zako, lakini fedha iliyobaki ipatikane haraka iwezekanavyo ili mradi huu ukamilike kwa wakati,” amesema.

Mhe. Mtanda amehitimisha kwa kusema kuwa yuko tayari kufuatilia kwa karibu utekelezaji wa mradi huo ili kuhakikisha fedha zinazotengwa zinatumika ipasavyo na kuleta matokeo yaliyokusudiwa.

Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.