Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda amemtaka mkandarasi HUMPHREY CONSTRUCTION LIMITED kuongeza kasi ya ujenzi wa jengo la ghorofa tano katika Hospitali ya Wilaya ya Nyamagana kwa kufanya kazi usiku na mchana ili mradi huo uanze kutoa huduma haraka.

RC Mtanda amesema Serikali imetoa zaidi ya shilingi bilioni 2 kwa mradi huo, huku mkandarasi akiwa tayari amechukua zaidi ya milioni 900, lakini kasi ya utekelezaji hairidhishi na idadi ya wafanyakazi ni ndogo.

Kwa mujibu wa mkataba, mradi ulipaswa kukamilika Januari mwaka huu, lakini hadi sasa umefikia takribani asilimia 83 ya utekelezaji. RC amemtaka mkandarasi kuhakikisha ifikapo tarehe 11 Machi anakamilisha awamu ya kwanza kama ilivyokubaliwa.

Ameonya kuwa kushindwa kutekeleza mradi kwa wakati kutasababisha mkandarasi huyo kukosa awamu ya pili na hatua za kisheria zitachukuliwa.

Vilevile, amemtaka Mkandarasi Mshauri, ATC Production and Consulting Bureau PLC ya Arusha, kutoa taarifa za mara kwa mara za maendeleo ya mradi na kusimamia ubora ili kuepuka kasoro za ujenzi.

Akitoa taarifa ya mradi, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Nyamagana, Dkt. Halima Basila amesema jengo hilo litatoa huduma za dharura, ICU, maabara, mionzi, upasuaji, kliniki za macho na meno, wodi za wazazi, wodi binafsi pamoja na ofisi za utawala.

Mradi huo wa siku 365 ulianza Novemba 2024. Hadi sasa zaidi ya shilingi milioni 826 zimetumika kwa mkandarasi mshauri na mjenzi, huku gharama ya mradi mzima ikikadiriwa kufikia zaidi ya shilingi bilioni 14. Serikali Kuu imeshatoa zaidi ya shilingi bilioni 2 kwa awamu mbili kusaidia utekelezaji wake.

Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.