Mganga Mkuu Mkoa wa Mwanza Dkt. Jesca Lebba jana Januari 31. 2026 amezindua kambi ya kupima afya iliyoandaliwa kwa ushirikiano kati ya Chama cha Wanafunzi wa Udaktari Tanzania (TAMSA) pamoja na taasisi ya The desk and chair foundation na yenye lengo la kupima afya na kutoa ushauri nasaha kwa wananchi.

Akizungumza baada ya kuzindua kambi hiyo iliyofanyika Mkoani Mwanza Dkt. Lebba ameshiriki zoezi la kuchangia damu huku akitoa wito kwa wananchi kujenga tabia ya kupima afya mara kwa mara ili waweze kujua hali zao za afya pamoja na kupata ushauri nasaha kutoka kwa wataalamu.

Aidha, ameongeza kwa kuwataka wananchi kua wanajitokeza kwa wingi katika kambi za matibabu ambapo zimeandaliwa na wataalamu huku akisistiza kua kupima afya ni muhimu kwani inasaidia katika kuchukua hatua stahiki na kwa wakati.

Sambamba na hayo Dkt. Lebba amewapongeza wanafunzi hao kwa kuandaa kambi ya uchunguzi kwa kushirikiana na wadau kwani kambi hiyo imeweza kuwagusa wananchi mbalimbali ambao hawakua na uwezo wa kufika hospitali kuangalia afya zao.

Kadhalika amewahamasisha wananchi kujiunga na huduma ya bima ya afya kwa wote ambayo itasaidia katika upatikanaji wa huduma kwa watu wote pamoja na kupunguza gharama za matibabu.

Kambi hiyo ya matibabu ni sehemu ya kusogeza huduma za afya karibu na wananchi huku kauli mbiu yake ikiwa ni ‘Anza mwaka kwa kujua afya yako’.

Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.