Serikali kupitia Baraza la Ushindani (FCT) imeendesha semina kwa wadau wa Mkoa wa Mwanza, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuimarisha ufanisi wa utekelezaji wa sheria za ushindani.

Semina hiyo imefanyika leo Februari 05 katika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza ikujumuisha wadau kutoka sekta mbalimbali za biashara.

Akifungua semina hiyo, Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza Bw. Balandya Elikana amesema kwamba semina hiyo ni muhimu kwa wadau wa sekta ya biashara kwa kuwa itawawezesha kuelewa vyema majukumu ya Baraza la Ushindani na umuhimu wa kuendeleza mshikamano katika utekelezaji wa sheria za ushindani.

Amesema kuwa, “Kupitia semina hii, tutapata uelewa mpana zaidi wa Baraza la Ushindani na umuhimu wa kulinda haki za mlaji na kuendeleza ushindani wa haki katika soko.”

Baraza la Ushindani (Fair Competition Tribunal – FCT) ni taasisi ya serikali iliyo chini ya Wizara ya Viwanda na Biashara. Lengo lake kuu ni kutatua migogoro ya kiushindani kwa njia ya rufaa kutoka kwa taasisi za udhibiti kama vile Tume ya Ushindani (FCC), EWURA, LATRA, TCAA, na TCRA. Ameongeza Katibu Tawala huyo.

Bw. Elikana ameeleza kuwa semina hiyo itawanufaisha washiriki kwa kuimarisha ufahamu wao kuhusu haki na wajibu wao katika masuala ya ushindani, na hivyo kuongeza uwajibikaji katika utekelezaji wa sheria.

“Serikali itaendelea kutoa ushirikiano wa kutosha ili kuhakikisha soko linakuwa na ushindani wa haki na linamlinda mlaji,” ameongeza.

Wadau wamehamasishwa kutoa maoni na ushauri kuhusu kuboresha mawasiliano kati ya Baraza la Ushindani na wadau wa sekta mbalimbali, ili kufanikisha malengo ya kuongeza ufanisi na uwazi katika soko.

Serikali kupitia Baraza la Ushindani imesema itaendelea kuwa na ushirikiano wa karibu na wadau wote ili kuhakikisha utekelezaji wa majukumu yao unafanikiwa na soko linakuwa na ushindani wa haki.

Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.