Waziri Mkuu wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba leo Januari 23, 2026 ameweka jiwe la msingi katika mradi wa ujenzi wa kituo cha kusukuma maji na maatenki ya kuhifadhia maji unaotekelezwa katika mtaa wa Sahwa kata ya Lwahnima jijini Mwanza.

Akizungumza katika hafla hiyo fupi ya uwekaji wa jiwe la msingi Mhe. Waziri Mkuu amewataka wakandarasi wanaotekeleza mradi huo kufanya kazi usiku na mchana ili kuhakikisha unakamilika kwa haraka kwa lengo la kuondoa kero ya maji kwa wananchi, akisisitiza kuwa serikali itakua macho kuwasimamia.

Ameongeza kwa kumuagiza waziri wa maji kuhakikisha kuwa fedha za zinazotoka kwaajili ya miradi ya maji zinakwenda kwenye miradi kwa haraka kwa sababu maji kama huduma ya kijamnii haina mbadala kwa wananchi kutokana na umuhimu wake mkubwa.

Akimkaribisha Waziri Mkuu, Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso (MB) amesema atashirikiana na Katibu Mkuu wa wizara yake kuhakikisha wanamsimamia mkandarasi ili mradi uweze kukamilika ndani ya muda kama mkataba unavyosema.

Awali akisoma taarifa ya mradi Mkurugenzi wa Mamlaka ya majisafi na usafi wa mazingira (MWAUWASA) Nelly Msuya amesema mradi huo unaotekelezwa na mkandarasi SINOHYDRO CORPORATION LIMITED & HIGHLAND BUILD CO., LTD (JV) ni sehemu ya programu ya Maji na Usafi wa Mazingira ya Ziwa Victoria (LVWATSAN), yenye lengo la kuboresha huduma ya upatikanaji wa majisafi pamoja na usafi wa mazingira kwa Jiji la Mwanza na maeneo jirani.

Aidha, amebainisha kuwa mradi huo unatarajiwa kuwanufaisha wakazi zaidi ya 450,000 jijini Mwanza, Magu na Misungwi katika maeneo ya Nyegezi, Mkolani, Buhongwa, Nyamazobe, Nyahingi, Buganda, Luchelele, Lwanhima, Sahwa, Fumagila, Kishiri na Igoma, wakati katika Wilaya za Magu na Misungwi mradi utanufaisha wakazi wa Kisesa, Bujora, Kanyama, Fela na Usagara kwa kupata huduma ya maji safi na ya uhakika, jambo ambalo litachangia kupunguza magonjwa yatokanayo na matumizi ya maji machafu.

Mradi huo ulianza rasmi kutekelezwa mwezi Juni, 2024 na unatarajia kukamilika mwezi Desemba, 2026 huku gharama za utekelezaji wa mradi huo ni zaidi ya Tsh. bilioni 46.

Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.