Askari wa jeshi la magereza,Kibemba Warioba (27) mwenye namba B.9205 WDR amekamatwa na jeshi la polisi mkoani Mwanza kwa kosa la kuanzisha saccos ya info tell CCM na kuwatapeli wanachama wa chama cha mapinduzi(CCM).
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Mwanza,Kamanda wa Polisi wa Mkoa huo,Jumanne murilo alisema askari huyo alikamatwa juzi baada ya kupokea malalamiko ya wanachama wa CCM kwamba kuna saccos ya info Tell CCM inatoa gawio zuri na kubadili maisha haraka ya wanachama.
Kamanda Murilo alisema baada ya taarifa hiyo kupokelewa, askari wa Mwanza walishirikiana na askari wa Mkoa wa Kagera walifuatilia mwanzilishi wa saccos hiyo na kufanikiwa kumkamata askari huyo wa magereza akiwa na laini za simu tano zikiwa zimesajiliwa kwa majina tofauti tofuati.
“Mtumishi huyo ameichafua sura ya jeshi la magereza, serikali, amechafua jina la chama cha CCM, hatuwezi kuvumilia watu wa aina hii kuendelelea kufanya uhalifu na utepeli, tutawashughulikia na kama kuna watu wenye nia ya kujihusisha na shughuli isiyo halali ni vema wakaiacha,”alisema.
Alisema baada ya uchunguzi dhidi ya askari huyo wa magereza alikiri ndiye mhusika na tayari amewatapeli wanachama wa CCM wengi na watu wengine wa kawaida huku akitambulisha kwa vyeo mbalimbali vilivyopo ndani ya CCM na serikali.
“Shughuli hii si kwamba alikuwa anaifanya yeye mwenyewe bali na watu wengine na baadhi tumewakamata ambao wamewatapeli wanachama wa CCM wakiwaeleza kuwa watapata gawio zuri na maisha yao yatakuwa mazuri na bora”alisema Murilo.
Hata hivyo Kamanda Murilo aliwataka wanachama wa CCM na watu wengine ambao wametapeliwa na saccos ya Info Tell CCM kufika katika vituo vya polisi kutoa taarifa zao ili waweze kurejeshewa fedha zao na hata kutoa ushahidi pale mtuhumiwa atakapofikishwa mahakamani.
Wakati huo huo watu 29 wanashikiliwa na jeshi la polisi mkoani humo kwa makosa mbalimbali yakiwamo mauaji ya wavuvi, wizi, unyang’anyi na upatikanaji wa dawa za kulevya aina ya bangi na mirungi.
Kamanda Murilo alisema miongoni mwa watuhumiwa hao, wapo watu wawili ambao ni wavuvi wamekamatwa kwa tuhuma za mauaji katika kisiwa cha Ukara baada ya kuwavamia wavuvi wenzao wawili ambapo waliwafunga kamba miguuni na mikononi na kuwatumbukiza ziwani.
Alisema katika tukio hilo, mvuvi mmoja kati ya wale waliofungwa kamba aliweza kupoteza maisha huku wavamizi wakiwapora injini ya boti, kokoro moja la dagaa, tanki la mafuta, simu na vitu mbalimbali vyote vikiwa na thamani ya zaidi ya sh milioni tano.
Vile Kamanda Murilo alisema katika operesheni ya juzi mkoani Mwanza, polisi walifanikiwa kuwakamata watu watano kwa kosa la kupatikana na vifaa vya kutengeneza noti za fedha bandia za Tanzania na dola ya Marekani.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.