Serikali imeeleza kuwa utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 iliyozinduliwa rasmi mwaka 2025, unaweka mkazo mkubwa katika kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji ili kuifanya Tanzania kuwa miongoni mwa nchi tatu bora Afrika kwa kuvutia mitaji, huku mikoa ya Kanda ya Ziwa ikitajwa kuwa nguzo muhimu ya safari hiyo ya mageuzi ya uchumi.

Hayo yamesemwa Jijini Mwanza na Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Judith Salvio Kapinga (MB), wakati wa Kongamano la Uwekezaji kwa Mikoa ya Kanda ya Ziwa, lililoandaliwa kama sehemu ya Kampeni ya Kitaifa ya Uhamasishaji Uwekezaji wa Ndani yenye lengo la kuchochea ushiriki mpana wa Watanzania katika uwekezaji.

Mhe. Kapinga amesema uwekezaji ni nyenzo muhimu ya kutatua changamoto za kijamii na kiuchumi kwa kuvutia mitaji, kuleta teknolojia ya kisasa, kuongeza ajira kwa vijana, kukuza ujuzi wa rasilimali watu, kuongeza mapato ya kodi na yasiyo ya kodi, kuongeza uzalishaji wa bidhaa na kuokoa fedha za kigeni zinazotumika kuagiza bidhaa kutoka nje ya nchi.

Amefafanua kuwa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inalenga kujenga Taifa jumuishi, lenye ustawi, haki na linalojitegemea, kupitia nguzo tatu na vichocheo vitano, huku nguzo ya kwanza ikilenga kujenga uchumi imara, jumuishi na shindani kwa kuimarisha mazingira wezeshi ya biashara na uwekezaji.

Ameitaja Taasisi ya Uwekezaji na Maeneo Maalum ya Kiuchumi Tanzania (TISEZA) kama mhimili mkuu wa utekelezaji wa Dira 2050 katika eneo la uwekezaji, akisema taasisi hiyo ndiyo mtafsiri wa maono ya Taifa kwa vitendo, kufuatia kuunganishwa kwa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) na Mamlaka ya Maeneo ya Uzalishaji kwa Mauzo ya Nje (EPZA) chini ya Sheria ya mwaka 2025.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda amesema utekelezaji wa kampeni hiyo katika Kanda ya Ziwa utaongeza kasi ya uwekezaji wa ndani, akibainisha kuwa mikoa ya kanda hiyo inachangia takribani asilimia 25 ya Pato la Taifa, hivyo miradi ya uwekezaji itakayotekelezwa itaongeza zaidi mchango wake katika ukuaji wa uchumi wa Taifa.

Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.