Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe.John Mongella amefungua kikao kikao kazi cha kwanza cha bodi ya Barbara ya Mkoa wa Mwanza cha mwaka wa fedha 2020/2021 na kusema kuwa kwa kipindi cha miaka mitano ijayo Mwanza itakuwa na sura mpya tofauti kutokana na viongozi waliopo kwa sasa hivyo mshikamano unahitajika ili kuimarisha miundombinu ya mkoa kwani serikali imetoa fedha nyingi za kutekeleza miradi mbalimbali.
Amesema kwa miaka mitano iliyopita wamefanikiwa katika sekta ya elimu siri ya mafanikio hayo ni uchapakazi ,umoja na utendaji kazi wenye tija ambao ulichangia watoto wote waliochaguliwa walifanikiwa kujiunga na shule hivyo hata kwa walichaguliwa kwa mwaka huu lazima wote wataingia madarasani, viongozi wote wafanye Kazi ili kuijenga nchi.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Magu Mhe.Salum Kalli na Mbunge wa Jimbo la Magu Mhe.Boniventura Kiswaga, walisema barabara ya Mahaha- Bariadi inaunganisha Mkoa wa Mwanza na Simiyu hivyo waliomba kujengwa kwa daraja ili kuweza kuunganisha mikoa hiyo na wananchi waweze kufanya shughuli zao za kimaendeleo .
Naye Mbunge wa Sumve Kasalali Mageni alisema kuna madaraja matatu ambayo mvua ikinyesha maji yanapita juu yake hivyo kufanya wananchi kupita kwa kudra za Mungu na ameiomba TARURA kuyapa kipaumbele madaraja hayo.
Akizungumzia utekelezaji wa Kazi na matengenezo ya barabara wakala wa TARURA Mkoa wa Mwanza Mhandisi Gaston Paschal amesema wanashughulikia matengenezo ya barabara za Mjini na vijijini katika Halmashauri Magu, Misungwi, Ukerewe,Buchosa, Sengerema, Kwimba, Ilemela na jiji la Mwanza hivyo kwa mwaka wa fedha 2020 hadi 2021 kwa Mkoa wa Mwanza wamepangiwa bilioni 11.2.
Ameongeza kuwa halmashauri zote zina mtandao wa barabara jumla ya 8628.039Km hadi Disemba 2020 kulingana na uthibitisho wa mtandao wa Wizara ya ujenzi uchukuzi na mawasiliano, nje ya mtandao huo barabara za lami ni 72.89 km, barabara za changarawe ni 1286.16km, barabara za udongo 7253.156 km,zege zikiwa 4.795km na za mawe zikiwa ni 11.03km.
Aidha, ameeleza matatizo yanayowasibu ni pamoja na wananchi kufanya shughuli za kibinadamu ,kilimo katika maeneo ya hifadhi pamoja na kiwango kidogo cha fedha za matengenezo ukilinganisha na Hali halisi ya mahitaji ya matengenezo ya barabara.
" Wizi na hujuma za alama za barabarani,makalavati,vyuma vya madaraja ,taa za barabarani,betri ,waya za umeme ,uchimbaji wa wananchi kupitisha mifugo barabarani, magari mazito kutumia barabara za viwango vidogo hayo yote ni matatizo" amesema Mhandisi Paschal.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.