Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda amefungua rasmi mafunzo ya awamu ya kwanza kwa Waheshimiwa Madiwani waliochaguliwa katika Uchaguzi wa Oktoba 2025 kutoka Halmashauri za Jiji la Mwanza, Manispaa ya Ilemela, pamoja na Halmashauri za Magu na Ukerewe.

Akizungumza wakati wa ufunguzi, Mhe. Mtanda amesema mafunzo hayo yamelenga kuwajengea uwezo madiwani katika maeneo ya msingi ikiwemo uongozi na utawala bora, sheria za uendeshaji wa serikali za mitaa, uendeshaji wa vikao vya kisheria, uandaaji wa mipango, bajeti, pamoja na usimamizi wa watumishi na miradi ya maendeleo.

Amesisitiza kuwa bado kuna dhana potofu miongoni mwa viongozi na wananchi kuwa usimamizi wa miradi ni jukumu la Wakuu wa Mikoa au Wilaya pekee hali inayosababisha baadhi ya miradi ya maendeleo kutotekelezwa ipasavyo, huku madiwani wakidhani ni jukumu la wahandisi au wakurugenzi.

Mhe. Mtanda amewahimiza Madiwani kutambua kuwa utekelezaji wa miradi katika maeneo yao ndiyo msingi wa uaminifu wao kwa wananchi, akisisitiza umuhimu wa kusimamia miradi, kutoa taarifa pale panapobainika dosari, na kuhakikisha fedha za maendeleo zinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa.

Pia ametoa wito kwa Wakufunzi kuweka kipengele cha uelewa wa mahusiano kati ya Halmashauri na Sekretarieti za Mikoa, pamoja na mipaka ya majukumu kati ya madiwani na watendaji wa serikali katika ngazi ya kata, ili kuepusha migongano na kuimarisha utendaji kazi wa pamoja.

Kwa mujibu wa Mwakilishi wa Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI, mafunzo hayo yatatolewa kwa muda wa siku tatu na yatahusisha mada 11, zikiwemo uongozi na utawala bora, muundo na madaraka ya serikali za mitaa, pamoja na uendeshaji wa vikao na mikutano ya kisheria.

Mada za mipango, bajeti, usimamizi wa miradi na udhibiti wa fedha zinalenga kuwajengea madiwani uwezo wa kusimamia rasilimali za umma kwa ufanisi.

Katika hatua nyingine, Mhe. Mtanda ametoa maelekezo kwa Halmashauri ambazo bado hazijafikia kiwango cha asilimia 80 ya matumizi ya mashine za POS, ikiwemo Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema, kukamilisha ununuzi wa mashine hizo ndani ya miezi mitatu na kuwasilisha taarifa ya utekelezaji.

Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.