Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza limesema tayari limenasa mtandao wa mafundi simu ambao wananunua simu za wizi zenye thamani kubwa na kwenda kuziuza au kubadilishana na wahalifu wa nchi jirani na Kenya ambao hukutana mpakani.
Akijibu maswali ya wadau mbalimbali katika simina iliyoandaliwa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kwa watoa huduma za mawasiliano nchini, Mussa Zuberi kutoka kitengo cha makosa ya mitandao Mkoa wa Mwanza, alisema mtandao huo umebainika baada ya kuanza kuwakamata mafundi simu na kuwahoji.
Alisema kwamba baada ya jeshi la polisi kupokea kesi nyingi za upotevu wa simu na kufuatilia ilibainika hupelekwa kwa mafundi simu ambao huziondoa namba ya siri na kubadilisha namba ya utambulisho yaani IMEI kwa matumizi.
TCRA imeandaa simina kwa wadau mbalimbali wakiwamo kampuni za mawasiliano Tanzania, viongozi wa umoja wa mafundi simu, waandishi wa habari, viongozi wa dini na wadau wengine wa sekta hiyo ikiwa lengo ni kukumbushana taswira ya sheria ya makosaya mitandao ya mwaka 2015 na changamoto zinazojitokeza.
Zuberi alifafanua kwamba baadhi ya simu zingine ambazo mafundi hao huzinunua huzipeleka mpakani mwaka Kenya na Tanzania na kuziuza au kubadilishana na mafundi wa Kenya jambo ambalo huwafanya polisi kitengo cha mkoasa ya mitandao kupata ugumu wa kuzipata kwani huwa hazionekanani katika mfumo wa mtandao.
“Mpaka tunapozungumza sasa tayari baadhi ya mafundi wanashikiliwa kwa vitendo hivyo na wametueleza namna biashara hivyo inavyofanyika, wanakwenda kule mpakani Sirari upande wa Tanzania wanakutana na wenzao wa Kenya wanabadilishana au kuuziana hizo simu za wizi, ndio maana mtu anaweza kuleta malalamiko tukashindwa kuipata simu yake.
“Tunapoitafuta kwenya mfumo wa mtandao wetu haipatikani kwani inakuwa nje ya Tanzania lakini mtumiaji yule anapokuja upande huu huwa inasomeka kwa muda na kutoweka sasa inakuwa vigumu kuifuatilia kwani tunakuwa mbali na mhalifu.
“Kikubwa tunachowaomba mafundi simu watambua kitendo cha kuanza kuchokonoa simu kwa kufuta namba ya siri iliyowekwa na mhusika sambamba na IMEI ni kosa, kosa la pili ni kuuza mali za wizi, hivyo tumewataka kuacha biashara hiyo na kushirikiana na polisi kuwakamata wale wanaowapelekea simu,”alisema.
Zuberi alisema hivi sasa wanatarajia kukutana na watu wa idara ya uhamiaji kuona namna kufanya ukagazi mpakani Sirari mkoani Mara katika mabegi ya abiria na pale wanakuta mtu akiwa na simu nyingi ambazo hazimo katiba maboksi rasmi au kutokuwa na stakabadhi za manunuzi zinapaswa kushikiliwa kwa mahojiano zaidi.
Hata hivyo alisema baadhi ya watu walioibiwa simu zao hukata tamaa pale anapotakiwa kutoa ushirikiano ambapo alitoa wito kwa jamii kuwa waangalizi katika matumizi ya simu zao za mikononi kwa kuepuka matusi na kusajili laini ambayo taarifa zake si kweli.
Naye Mkuu Msaidizi wa Kitengo cha uhalifu wa kimtandao kutoka makao makuu ya jeshi la polisi, Joshua Mwangasa alisema tangu mwaka 2015 takwimu za makosa yamekuwa yakiongezeka na kupungua.
“Ukiangalia mwaka 2015 tulipokea makosa 5,172, 2016 (9,441), 2017 (7889) na mwaka 2018 tulipokea 8,708 hapo utaangalia yanapanda na kushuka lakini nasema tunakoelekea 2020 tunakwenda katika kiwango cha juu cha matumizi ya teknolojia ambacho kila mtu shughuli zake zitakuwa kwenye simu.
“Tukumbuke hata vitabu vitakatifu vimeandika siku za mwisho maarifa yataongezeka hivyo kuanzia mwaka 2020 watanzania wataanza kutumia kiwango cha 5GB, ni lazima sasa kama polisi na TCRA tukaanza kutoa elimu ya kuwalimisha namna ya kuepuka kuingia kwenye makosa ya jinai.
“Matokeo ya matumizi mabaya ya mtandao wa kijamii yamegawanyika sehemu tatu, kwa upande wa kijamiini unaleta mmomonyoko wa maadili, upande wa siasa inaleta uvunjifu wa amani na kundi la mwisho ni lipo kwenye uchumi na athari zake ni kuharibu mfumo muhimu wa kitaifa,”alisema.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.