MAGU KUFUNGA DIMBA MBIO ZA MWENGE WA UHURU MKOA WA MWANZA LEO
Halmashauri ya wilaya ya Magu, mapema leo tarehe 20 Julai, 2023 imepokea Mwenge wa Uhuru ukitokea Kwimba tayari kwa kuukimbiza kwenye miradi sita yenye thamani ya zaidi ya Shilingi Bilioni 1.6 na kuhitimisha kwa Halmashauri za Mkoa wa Mwanza.
Akizungumza kwenye mapokezi yaliyofanyika kwenye viwanja vya shule ya msingi Kabila, kaimu Mkuu wa Wilaya ya Magu Mhe. Hassan Masala amebainisha kuwa wapo tayari kukimbiza Mwenge wa Uhuru ambao unatarajiwa kukimbizwa kwenye miradi iliyoandaliwa kwenye ubora.
Mhe. Mkuu wa Wilaya amefafanua kuwa Mwenge wa Uhuru uwapo wilayani humo utakimbizwa kwenye eneo la umbali wa Kilomita 74 na kwamba wana shauku kubwa ya kuukimbiza ili umulike na kuangaza miradi ya wananchi ya maendeleo.
"Mwenge wa Uhuru utapokuwa kwenye Halmashauri yetu ya Magu utaweka jiwe la msingi kwenye mradi mmoja, utafungua mradi mmoja pamoja na kuzindua miradi minne yote ikiwa inang'ara na kupendeza." amefafanua Mhe. Masala.
Naye, Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru 2023 Ndugu Abdalla Shaib Kaim amenadi ushirikiano kuwa ndio nguzo itakayofanikisha mbio hizo wilayani Magu na ametoa wito kwa wana Magu kutofanya shughuli zozote jirani na vyanzo vya maji ili kutunza na kuhifadhi mazingira.
Masala amesema ni lazima jamii iachane na tabia za kuchoma misitu wakati wa kuandaa mashamba, kuacha uvuvi haramu, kuacha uchimbaji wa madini ambao unaharibu mazingira na kutofanya shughuli ndani ya mita 60 kutoka kwenye vyanzo vya maji ili kulinda uoto wa asili.
Kaulimbiu ya mbio za Mwenge wa Uhuru 2023 inasema "Tunza Mazingira, Okoa vyanzo vya Maji kwa Ustawi wa viumbe hai kwa Uchumi wa Taifa."
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.