*Katibu Mkuu Afya awataka Makatibu wa Afya Kusimamia huduma bora kwa Jamii*
Katibu Mkuu Wizara ya Afya Dkt. Seif Shekalaghe amewataka Makatibu wa Afya Nchini kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za afya kwa haraka, upole na unyenyekevu kila wakati.
Dkt. Shekalaghe amesema hayo leo Mei 17, 2023 wakati akifungua Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Chama cha Makatibu wa Afya Tanzania ambao kitaifa unafanyika Mkoani Mwanza kwenye ukumbi wa Gold Crest kuanzia Mei 16-19, 2023.
Amesema kabla ya Chama Cha Mapinduzi kupata ridhaa ya kuongoza nchi kilipeleka Ilani kwa wananchi kuwa watatoa huduma yenye viwango vya juu kwa wananchi na ndipo wananchi wakakichagua chama hicho na kuongoza Serikali.
"Wizara ya Afya imepewa jukumu la kuhakikisha huduma za afya zinafika kwa wananchi tena kwa ubora, ni mkataba wa kijamii uliowekwa baina ya wananchi na Serikali kupitia uchaguzi Mkuu uliofanyika kuchagua chama gani kitatuongoza." Dkt. Shekalaghe.
Vilevile, Katibu Mkuu ametumia wasaa huo kuwaahidi wanataaluma hao kushughulikia masuala ya uanzishwaji wa baraza la kitaaluma na katika kuboresha Muundo wa kada hiyo ameahidi kuzungumza kwa pamoja na Katibu Mkuu TAMISEMl ili kulipatia ufumbuzi mara moja.
Katika kuboresha huduma, Katibu Mkuu amewaagiza kubaini vikwazo vya watumishi kwenye utoaji wa huduma na kutoa Mapendekezo ya namna ya kuboresha na kwamba katika utendaji wao wajenge upendo baina ya watumishi na kuthamini mchango wa kila mmoja.
Ameongeza kuwa katika utoaji wa huduma za afya kila mmoja anapaswa kuwa na lugha tamu ya ufariji kwa mgonjwa kabla hata ya kumhudumia mgonjwa hivyo wanataaluma hao wanapaswa kwenda kusimamia duala hilo kila wakati ili kujenga jamii bora.
Naye, Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza Ndugu Balandya Elikana ametoa rai kwa Makatibu wa Afya kusimamia maadili ya utumishi wa umma kwa kuwasimamia watoa huduma ili kuwahakikishia wananchi upatikanaji wa huduma bora za afya na kuitendea haki Miundombinu iliyoboreshwa na Serikali.
Awali, Mwenyekiti wa Chama cha Makatibu wa Afya Bi. Juliana Mawala amebainisha changamoto za kutokua na Baraza kukwamisha usimamizi wa masuala ya kinidhamu kwa watumishi wa afya na Muundo Mpya kutomtambua katibu wa afya kama Msimamizi Mkuu wa masuala ya wafanyakazi wa kada ya afya kukwamisha kazi zao.
Akitoa historia ya Chama Cha Makatibu wa Afya nchini Dkt. Anna Nswila amebainisha kuwa taaluma hiyo duaniani ilianza miaka ya 1940 na baada ya Uhuru Serikali iliona umuhimu wa Utawala na Rasilimali watu kwenye Sekta ya Afya badala ya kuachwa shughuli hizo kuendelea kufanywa na Matabibu kama ilivyokua awali.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.