Mhe Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhe Mhandisi Robert Gabriel ametoa rai kwa Vikundi vilivyofuzu kupata ruzuku kwa ajili ya kuendesha biashara katika kupambana na athari zitokanazo na ugonjwa wa Uviko 19 kuzingatia malengo ya mradi ili kufikia malengo.
Amesema hayo mapema leo kwenye Ukumbi wa Nyerere-Gold Crest Hotel wakati wa hafla ya Utoaji Ruzuku ya zaidi ya Tshs Milioni 169 kwa vikundi 90 vya huduma ndogo ya fedha iliyoratibiwa na Shirika la Aga Khan Foundation mradi unaolenga kupambana na athari za Ugonjwa wa Uviko 19 kwa jamii.
"Kipekee kabisa naomba nimshukuru Mhe. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia awamu ya Sita ya uongozi wake kwa kuendelea kuimarisha mahusiano ya kidiplomasia na nchi mbalimbali ikiwemo Umoja wa Ulaya ambao pia wamefadhili mradi huu wakishirikiana na Shirika la Aga Khan Foundation." Mkuu wa Mkoa.
"Hii ni fursa kubwa sana kwa mkoa kwa kupatiwa usaidizi wa kitaalamu na kifedha katika kuhakikisha wananchi wetu wanajengewa uwezo hivyo ni lazima mdhihirishe kwamba kule kuaminiwa kwenu kunaleta taswira kwamba Mwanza mradi ukileta unatekelezeka." Mhandisi Gabriel.
"Naomba niwasihi wanavikundi wote kuwa ruzuku hizi sio kwa ajili ya kufanyia sherehe au kujengea nyumba, mnapewa fedha kwa ajili ya kuendesha biashara zenu katika kujiinua kutoka kwenye umasikini." Simon Meigaro, Kaimu Mkurugenzi Mkazi The Aga Khan Foundation.
Mratibu wa mradi wa utoaji ruzuku kwa vikundi vya huduma ndogo ya fedha, Japhet Wange amesema vikundi vyote vilivyopo kwenye mradi huo vitapata ruzuku ya zaidi ya Milioni 169 na vinaanza rasmi kazi na kwamba mradi upo kwenye mfumo wa hisa ambazo zitaendeshwa kwa kutumia simu katika kufikia malengo.
"Mhe Mkuu wa Mkoa tuliandaa utaratibu wa kupata vikundi hivi na tunashukuru ofisi za Maafisa maendeleo za Halmashauri na Mkoa kwa usaidizi na hapa leo tupo na vikundi vya wawakilishi 90 ambavyo ndivyo vinaenda kupokea ruzuku hizi," amebainisha Wange.
"Vilevile, Mradi wetu unafanya kazi na vijana wajasiriamali na tunao vijana 100 kutoka kwenye mkoa huu ambao watajengewa uwezo wa kuboresha biashara zao ili waweze kujiinua na kuwaajiri hata vijana wenzao kwenye jamii." amefafanua.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.