Mkoa wa Mwanza umeishachukua hatua mbalimbali ili kukabiliana na homa inayosababishwa na Virus vya Marburg ikiwemo kuwapa watumishi wa afya mafunzo mahususi ya kuhudumia wagonjwa, kutenga maeneo maalum ya kuwahudumia wagonjwa wa ugonjwa huo na kuwaelimisha wananchi kuhusu ugonjwa wa Marburg na jinsi ya kujikinga.
Ikumbukwe kwamba Machi 21, 2023 Waziri wa Afya Ummy Mwalimu alitoa taarifa kwa Umma kwamba uchunguzi wa kimaabara uliofanyika katika Maabara ya Taifa ya Jamii umethibitisha uwepo wa ugonjwa wa homa inayosababishwa na Virus vya Marburg mkoani Kagera ambapo kulikuwa na juma ya wagonjwa nane kati yao watano walifariki na watatu wanaendeleana matibabu katika vituo vya kutolea huduma za afya vilivyoandaliwa Mkoani humo.
Akizungumza leo Machi2 4,2023 kwenye kikao kilichokutanisha wadau mbalimbali wakiwemo viongozi wa dini, wavuvi, na machinga kilicholenga kuwaelimisha kuhusu ugonjwa huo, dalli, jinsi ya kujikinga, unavyoambukizwa na athari zake, Mratibu wa Elimu ya Afya kwa Umma Mkoa wa Mwanza, Renard Mlyakado amesema hadi sasa jumla ya watumishi 94 kutoka Wilaya nne kati ya saba zilizopo mkoani humo wamekwishapata mafunzo jinsi ya kuhudumia wagonjwa wa ugonjwa huo na mafunzo yanaendelea katika halmashauri zote na mahala pa kazi.
"Pia halmashauri zote zilizopo mkoani humu zimekwishatenga maeneo maalum ya kuhudumia wagonjwa wa ugonjwa wa Virus vya Marburg ambapo Nyamagana ni Hospitali ya Wilaya na SRRH,Ilemela ni Hospitali ya Wilaya Kabusungu, Kwimba zahanati ya Mwamajila, Misungwi Zahanati ya Igokello, Buchosa ni Hospitali ya Wilaya, Ukerewe ni hospitali ya Nansio na Bwisya, Sengerema ni zahanati ya Mwabaluhi na Magi ni zahanati ya John Mongela," ameeleza Mlyakado.
Akieleza namna ugonjwa huo unavyoambukiza Mlyakado amesema unaambulizwa kwa haraka kutoka mtu mmoja aliye na Virus vya Ugonjwa huo hadi mwingine kwa kugusa majimaji ya mwili mfano damu, matapishi, mkojo, jasho, machozi na kamasi,kugusa au kuosha maiti ya mtu aliyefariki kwa ugonjwa huo, kugusa godoro,shuka, blankenti au nguo zilizotumiwa na mgonjwa wa Ugonjwa wa Virus vya Marburg.
"Ugonjwa huu pia unaambukizwa kwa kuchomwa sindano au vifaa visivyosafi na salama vilivyotumiwa na ugonjwa wa Virus vya Marburg, kugusa mizoga au kula wanyama pori kama vile nyani,polo na sokwe na kula matunda yaliyoliwa nusu na wanyama" ameeleza na kutaja dalili za ugonjwa huo.
"Dalili huanza kujitokza kati ya Siku mbili hadi 21 baada ya mtu kupata maambukizi ikiwemo homa Kali ya ghafla, maumivu ya kichwa, mwili, misuli na viungo vya mwili, kuharisha na kutapika kunakoweza kuambatana na damu, vipele mwilini, kuvia damu chini ya ngozi au kutokwa na damu puani, mdomoni,machoni na masikioni," amebainisha Mlyakado.
Mlyakado amesema ugonjwa huo hauna tiba maalum wala chanjo bali ugonjwa hupatiwa tiba saizi kulingana na dalili alizonazo ambapo alisisitiza kwamba ili kukabiliana na mlipuko wa Ugonjwa wa Virus vya Marburg kila mtu na sekta ashiriki na atimize wajibu wake kwa kushirikiana na wataalamu wa afya katika kutoa elimu kwa Umma juu ya ugonjwa huo.
Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza, Mbunifu wa Majengo Chagu Ng'homa ameitaka jamii kutokuwa na hofu kwa kuwa Mkoa huo umejipanga kukabiliana na kuingia kwa ugonjwa huo ikiwa ni pamoja na kutoka elimu kwa wananchi jinsi ya kujikinga ili wasipate maambukizi.
"Tunatakiwa tupambane na hili janga bila kuleta taharuki kwa jamii natambua kwamba Ugonjwa wa Virus vya Marburg husababisha unyanyapaa na athari za kisaikolojia kwa waathirika na familia zao na pia ni gharama kubwa kuhudumia wagonjwa wa ugonjwa huo lakini ni lazima tushirikiane tusiwe na hofu Serikali inaendelea kuchukua hatua mbalimbali hasa kule Mkoani Kagera ulikoanzia hii inatupa matumaini na hatujatangaziwa ongezeko la wagonjwa," alisema Ng'homa.
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mwana Dkt.Thomas Rutachunzibwa alisema endapo MTU atakuwa na dalili moja wapo kati ya zilizotajwa au akiona MTU kwenye dalili hizo asimnyanyapae bali waende au wawashauri kwenda haraka kwenye vituo vya kutolea huduma za afya, watoe taarifa mapema kwenye vituo cha huduma za afya, oisi ya Serikali ya Mtaa au Kijiji.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.