Mkurugenzi Idara ya Menejimenti ya Maafa kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu Brigedia Jenerali Hosea Ndagala leo tarehe 20 februari, 2026 amefunga mafunzo yaliyotolewa kwa siku 5 kwa timu ya kukabiliana na dharula mkoni Mwanza.

Akizungumza wakati wa hafla fupi ya ufungaji Brigedia Ndagala amewataka wajumbe wa timu hiyo kuhakikisha wanauhisha taarifa za masuala ya maafa kwa wakati na kuelimisha jamii juu ya dharula na namna ya kukabiliana.

Aidha, amewataka wajumbe kuhakikisha wanatumia nyenzo za asili zinazopatikana kwa wananchi kuelewa njia rahisi za kukaniliana na maafa pamoja na dharula bila kusubiri msaada wa vifaa kutoka nje ambavyo vinaweza kuchelewa kutokana na asili ya janga.

“Tukizitumia redio zilizopo hapa wananchi wa chini kabisa watapata taarifa kwa wakati na watajiandaa dhidi ya janga linalokwenda kutokea ambalo limetolewa taadhari mathalani kama kuna mlipuko wa magonjwa ya mlipuko kama kipindupindu.” Amefafanua.

Ameongeza kuwa Ofisi ya Waziri Mkuu inaendelea kuboresha mifumo inayolenga kujenga jamii stahimilivu dhidi ya majanga na kuhakikisha vituo vinavyojengwa kwenye mikoa vinakuwa na wataalamu pamoja na vifaa vya dharula vya kutosha kwa kushirikiana na mdau UNDP.

Naye, Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa huo Bw. Daniel Machunda ametumia wasaa huo kuishukuru ofisi ya Waziri Mkuu na ameahidi kuwa wajumbe watakuwa nyenzo ya kupunguza majanga ya Asili na yanayosababishwa na binadamu kutokana na uwezo waliojengewa.

Mwakilishi kutoka UNDP Bw. Abas Kitogo ameishukuru Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kushirikiana na Shirika hilo huku akibainisha kuwa kwa kipindi kirefu wamekuwa wadau wakubwa wa miradi mbalimbali nchini na kwamba uwepo wa kituo hicho ni muendelezo wa vituo vingine kama kilichojengwa Jijini Dodoma.

Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.