MWANZA WATOA MAONI YA NAMNA BORA YA KUKUSANYA KODI NCHINI
Mwenyekiti wa Tume ya Rais ya Kukusanya maoni ya maborehso ya kodi Mhe. Balozi Ombeni Sefue ametoa rai kwa wafanyabiashara Mwanza kujenga tabia ya kulipa kodi ili kuipa nguvu Serikali na kuhakikisha inaweza kujitegemea kwa kuboresha miundombinu mathalani ya afya.
Ametoa wito huo leo Jumatatu tarehe 13 Januari, 2025 katika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wakati akifungua kikao cha wadau cha kukusanya, kupendekeza na kuwasilisha changamoto za masuala ya kodi nchini kilicholenga kuboresha namna bora ya pamoja ya kufikia malengo.
"Tanzania tija yetu ya kukusanya mapato bado ni ndogo ni kati ya asilimia 12 hadi 13 tu na haipaswi kuwa kuwa hivyo maana angalau tufikie asilimia 16 maana wananchi wanataka shule zijengwe, miundombinu ya afya iwepo tena ya kisasa je tutafikaje huko kama hatutakua na fedha." Mwenyekiti.
Mwenyekiti wa Chemba ya wafanya biashara Mwanza (TCCIA) Gabriel Chacha ametoa wito kwa Serikali kuondoa mfumo wa kukokotoa kodi ambao sio rafiki kwani haufuti taarifa za nyuma za uhai wa biashara na waondoe utitiri wa kodi kwenye biashara badala yake zilipwe kwenye mwamvuli mmoja.
"Changamoto nyingine ni sheria, faini na tozo hapa wafanyabiashara wanaumizwa sana na zinapaswa kupitiwa upya na kuzirekebisha maana adhabu zimewekwa kwa kiwango kimoja ambacho kinawaumiza moja kwa moja wajasiriamali." Ameongeza Bwana Chacha.
Wajumbe wengine wa tume hiyo ni Mhe. Balozi Maimiuna Tarishi Makamu Mwenyekiti wa Tume, Mhe. Balozi Mwanaid Maajar, Prof. Mussa Assad, Prof Florens Luoga, CPA. David Tarimo, CPA. Leonard Mususa, CPA. Rished Bade pamoja na CPA Abubakari Abubakar.
Tume hiyo imeundwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa ajili ya kupokea maoni ya wadau juu ya kuwa na mfumo bora wa kukusanya mapato nchini pasipo malalamiko.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.