Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda ametoa wito kwa Maafisa Ustawi wa Jamii pamoja na wadau wa makundi ya watu wenye ulemavu kuisaidia Serikali kuwabaini, kuwalinda na kuwatetea watu wenye ulemavu wanaofichwa au kutengwa majumbani.

Mhe. Mtanda ametoa wito huo leo Februari 06, 2026 wakati wa uzinduzi wa Kamati ya Ushauri ya Mkoa kwa ajili ya Watu Wenye Ulemavu, akisisitiza kuwa ni wajibu wa Serikali kuhakikisha kila mtu mwenye ulemavu anapata haki sawa na kushiriki kikamilifu katika jamii.

Amesema Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022 imebainisha kuwa Mkoa wa Mwanza una jumla ya watu 332,682 wenye ulemavu, sawa na asilimia 11.8 ya wakazi wote wa mkoa huo, hivyo ni kundi kubwa linalohitaji sauti na uwakilishi madhubuti.

“Ni kundi kubwa lenye mchango muhimu. Bila jukwaa la pamoja la kujadili changamoto na kupanga mipango yao, sauti zao haziwezi kufika serikalini. Ndiyo maana tumeunda kamati hii ili iwe daraja la mawasiliano,” amesema Mhe. Mtanda.

Aidha, amewaagiza Maafisa Ustawi kuhakikisha kamati na majukwaa kama hayo yanaanzishwa na kufanya kazi kuanzia ngazi za wilaya, kata hadi vijiji na mitaa, ili kuhakikisha masuala ya watu wenye ulemavu yanawasilishwa ipasavyo.

Vilevile, Mkuu wa Mkoa ameelekeza halmashauri zote kuhakikisha kamati hizo zinakaa mara kwa mara kujadili kwa kina masuala yanayohusu watu wenye ulemavu, huku mihutasari ikihifadhiwa kwa kumbukumbu na kutumika katika Kamati za Mikopo, MTAKUWWA pamoja na kuwasilishwa kwa Wakuu wa Wilaya kwa ajili ya ufuatiliaji wa karibu.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati Bw. Sibstain Meghjee amesema dhamira yao kuu ni kuishauri Serikali na taasisi binafsi, ikiwemo kutoa mapendekezo ya kisera yatakayolijengea nguvu kundi la watu wenye ulemavu na kuongeza ushiriki wao katika maendeleo ya Taifa.

Awali akizungumza katika uzinduzi huo, Afisa Ustawi wa Jamii Mkoa wa Mwanza Bw. Baraka Makona amesema Sheria ya Watu Wenye Ulemavu Sura Na. 9 ya mwaka 2010 inaelekeza kuundwa kwa Kamati za Ushauri kuanzia ngazi ya mkoa, halmashauri hadi vijiji na mitaa, kwa lengo la kuhakikisha watu wenye ulemavu wanajumuishwa kikamilifu katika mipango na maamuzi ya maendeleo.

Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.