Wadau na Wataalamu wa afya wametakiwa kuweka mkakati wa kuelimisha na kuhamasisha jamii kuchangia damu ili kusaidia kuokoa maisha ya watu.
Rai hiyo ilitolewa na Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza, Christopher Kadio, wakati akiwakabidhi vyeti wadau waliofanikisha uchangiaji damu kwenye maadhimisho ya siku ya damu yaliyofanyika mkoani Mwanza kitaifa , Juni mwaka huu.
Alisema ili kuokoa maisha ya wananchi wenye uhitaji wa damu wadau na wataalamu wa afya waweke mkakati endelevu wa kutoa elimu kwa jamii na kuhamasisha uchangiaji damu.
“Wataalamu wa afya mnatakiwa kulifanya zoezi la uchangiaji damu kuwa endelevu na hivyo mtafute jukwaa la kuelimisha jamii ili tufike mahali ijenge utamaduni wa kuchangia damu kwa hiari na kuweza kutatua changamoto hiyo,”alisema Kadio.
Pia alishauri kutokana na hospitali nyingi kumilikiwa na taasisi za dini ni vyema viongozi wa madhehebu ya dini wakawahamasisha waumini wao kuona umuhimu wa kutoa damu kwa maslahi ya jamii.
Awali Mkuu wa Huduma Maabara Mkoa wa Mwanza, Julius Shigela alisema wadau hao wametunukiwa vyeti hivyo ili kutambua na kuthamini mchango wao kutokana na mafanikio ya ukusanyaji na uchangaji damu.
Alisema Mkoa wa Mwanza katika maadhimisho ya damu duniani yaliyofanyika jijini humu Juni mwaka huu, ulifanikiwa kukusanya unit (chupa) 10,669 na kuvuka lengo la wizara kwa asilimia 203, kwa mkoa wakivuka kwa asilimia 101 la kukusanya chupa 4000.
Miongoni mwa wadau waliotunukiwa vyeti kwa niaba ya wengine zaidi ya 30 ni pamoja na The Desk & Chair Foundation,halmashauri za Jiji la Mwanza na Manispaa ya Ilemela, Isamilo Lodge,Aga Khan Foundation, hospitali za Pasiansi SDA,Hindu na CF.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.