RAS Mwanza ashauri ufugaji wa kisasa wa Samaki wa vizimba ufanyike kwa awamu ziwani
Leo Januari 11, 2024 Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza Balandya Elikana ameupokea ugeni Ofisini kwake kutoka Wizara ya mifugo na uvuvi ukiongozwa na Afisa Uvuvi Mkuu Bi. Mkonanile Mahundi.
Katika mazungumzo yao mafupi, Balandya ameipongeza Wizara hiyo kwa mkakati wenye tija wa kuwajengea uwezo vijana wa kujiajiri na kushauri mpango huo wa ufugaji kwa njia ya vizimba ufanyike kwa awamu kutokana na wingi wa vikundi husika kutoka mikoa ya kanda ya ziwa.
"Serikali ya Rais Samia imedhamiria kuwainua kundi la vijana kimaendeleo, mpango huu wa ufugaji wa kisasa wa samaki wataalamu kutoka wizarani ukiwawekea mazingira mazuri ya kazi utazidi kuwa na tija kwao kiuchumi", amefafanua Mtendaji huyo wa Mkoa wakati wa mazungumzo hayo.
Ameitaka Wizara ya Mifugo na Uvuvi kuweka ushirikiano na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa ili kuhakikisha miradi hiyo inafanyiwa ufuatiliaji na kuwa endelevu na mwishowe inafikisha ndoto ya Rais Samia kuona inawakomboa kiuchumi vijana.
Kwa upande wake Afisa Uvuvi Mkuu Bi. Mkomanile Mahundi amesema lengo la kuja Mwanza ni kukagua mchakato mzima wa mradi huo ikiwemo kukagua andiko la mkopo la mradi kutoka vikundi husika na kushauri pale zitakapo bainika changamoto ili zoezi hilo liwe limekamilika kabla ya Januari 29 2024.
"Tutapita maeneo yote Mikoa ya Kanda ya Ziwa ambayo mradi huu wa ufugaji wa samaki kisasa kwa njia ya vizimba unafanyika ili tujiridhishe kwa kila hatua kabla ya kuwakabidhi wahusika wote waliokidhi vigezo vya mradi huu",amesisitiza Bi.Mahundi
Mkoa wa Mwanza una jumla ya vikundi 79 wakiwemo watu binafsi 11, kampuni 6, vijana 13 na vikundi 49 huku Serikali ikiwa imetoa jumla ya Bilioni 65 kufanikisha mradi huo wa ufugaji samaki kwa njia ya vizimba ukiwemo pia kuwapatia wavuvi boti za kisasa.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.