RAS MWANZA AWATAKA WADAU WA MAAFA KUWA NA MIKAKATI YA KUKABILIANA NA ATHARI ZA EL NINO
Katibu Tawala Msaidizi Seksheni ya Uchumi na Uzalishaji Emily Kasagara amewataka wadau wa Maafa Mkoani Mwanza kujiandaa kwa kina kukabiliana na maafa ya mvua za El Nino zinazotarajiwa kunyesha siku za usoni ili kuwa na namna bora ya kuwalinda ili jamii isiangamie.
Akifungua leo tarehe 25 Septemba 2023 kikao kazi cha kujadili masuala ya maafa chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Idara ya Menejimenti ya Maafa kwa niaba ya Katibu Tawala wa Mkoa, Kasagara amesema ni lazima kamati za Maafa katika ngazi zote kuwa na mkakati kabambe wa kukabiliana nazo.
Aidha, ametoa wito kwa wadau hao watakaoketi kwa siku mbili za mjadala mzito wa namna ya kukabiliana na majanga kuchangia uzoefu wao na utaalam wao kwenye namna gani wanaona inafaa kukabiliana na hali hiyo itakapotokea na wafikishe elimu kwenye jamii ili kuikinga kwa pamoja.
Naye, Ndg. Prudence Costantine, Mkurugenzi wa Maafa kutoka Idara ya Menejimenti ya maafa-Ofisi ya Waziri Mkuu amesema Serikali kupitia Mamlaka ya Hali ya Hewa tarehe 24 Agosti, 2023 ilitoa utabiri ulioonesha kwamba kutakua na Mvua za wastani na juu ya wastani (El Nino) kwa mikoa kadhaa nchini ukiwemo Mkoa wa Mwanza hivyo ni lazima wadau wajiandae kukabiliana nazo.
"Tunaweza tukapata maafa kama magonjwa na vinginevyo kutokana na mvua hizo na ndio maana ofisi ya Waziri Mkuu ikaona ije na mpango wa kukabiliana na maafa hayo na hadi sasa wataalamu mbalimbali wamesambaa kwenye mikoa mbalimbali kuketi pamoja na kamati za maafa za mikoa hiyo kuona namna ya kukabiliana." Amesema Costantine.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.