RC MAKALLA AZINDUA MAJARIBIO YA CHANZO KIPYA CHA MAJI BUTIMBA, HUDUMA YA MAJI MWANZA KUIMARIKA
*Amshukuru Rais Samia kwa Kutoa zaidi ya Bilioni 69 za mradi huo*
*Atoa wito kwa Wabunge kufanya mikutano ya hadhara kuelezea uboreshaji mkubwa wa miradi ya Maji*
*Asema Mkandarasi wa kujenga mradi mwingine mkubwa kupatikana ndani ya muda mfupi*
*Awataka Wananchi kutoa taarifa MWAUWASA waonapo Maji yakivuja Mtaani*
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe.CPA Amos Makalla leo Septemba 15, 2023 amezindua Majaribio ya Chanzo Kipya cha Tiba ya Maji Butimba kituo ambacho kitazalisha Lita milioni 48 kwa siku kilichojengwa na Kampuni ya Sogea Satom chini ya usimamizi wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Mwanza (MWAUWASA).
Akizungumza na wananchi baada ya kubonyeza kitufe na kuwasha mitambo ya Maji na hivyo kuanzisha rasmi majaribio Mhe. Makalla amesema katika muda mfupi ujao wananchi wanaoishi katika maeneo ya Sahwa, Igoma, Kishiri, Nyamhongolo na Kisesa wataanza kupata Maji kutoka katika chanzo hicho kilichogharimu zaidi ya bilioni 69.
Mhe. Mkuu wa Mkoa ametumia hafla hiyo kumshukuru Mhe. Rais Samia kwa kuendelea kutoa fedha ili kutekeleza mradi huo unaotarajia kuongeza uzalishaji hadi lita milioni 138 kwa siku kutokana na chanzo cha sasa kuzalisha lita milioni 90 na miradi mingine inayolenga kuondoa kero ya Maji kwa wananchi Mkoani humo na wataalamu wote waliofanikisha ujenzi wa mradi huo.
Vilevile, Mhe. Makalla amebainisha kwamba kupitia mradi wa LVWATSAN kwa suluhisho la muda wa kati tayari zabuni kwa ajili ya ujenzi wa mtandao wa mabomba na Matenki makubwa sita yenye uwezo wa kuhifadhi maji jumla ya Lita milioni 31 imetangazwa na kwamba mkandarasi anatarajiwa kupatikana siku za usoni.
"Ndugu wananchi, napenda kuchukua fursa hii kuwaomba mnapoona maji yakivuja mtaani mtoe taarifa MWAUWASA nanyi mzishughulikie taarifa hizo kwa haraka na kwa umakini ili kuokoa maji, kuwatia moyo wananchi na kuzuia matatizo kama hayo yasijitokeze tena sehemu ileile." Mkuu wa Mkoa.
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa, Mhe. Sixbert Gichabu amesema chama tawala kina matarajio makubwa kwa Serikali yao na Mhe. Rais Samia ameamua kuwaletea huduma bora wananchi na ametoa pongezi kwa MWAUWASA kwa kutoa elimu kwa umma kila wakati juu ya maendeleo ya huduma za maji.
Naye, Mbunge wa jimbo la Nyamagana Mhe. Stansilaus Mabula ametumia wasaa huo kutoa shukrani kwa Rais Samia kutokana na jitihada za kuwaletea wananchi wake Maji safi na Salama huku akibainisha kuwa Mhe. Rais aliahidi mwenyewe kumaliza tatizo la maji jijini humo.
"Pamoja na jitihada hizi, iko haja ya kufumua mifumo na kuangalia mabomba yanayosambaza maji kama yanakidhi uwezo na kufanya ukarabati mara moja ili Miundombinu iende sambamba na mahitaji na kwakweli tunamshukuru sana Mhe. Rais Samia kwa kuwajali wananchi." Mhe. Angelina Mabula, Mbunge wa Ilemela.
Kaimu Mkurugenzi MWAUWASA, Bi. Nelly Msuya amesema mahitaji ya Maji jijini mwanza ni zaidi ya lita Milioni 165 kwa siku na kwamba chanzo cha zamani ambacho kinahuumia sasa cha Kapripoint kimekua kikizalisha Lita milioni 90 tu kwa siku hivyo Serikali kuona umuhimu kuongeza miradi mingine ili kuongeza uzalishaji.
"Kwa mujibu wa Mkataba ifikapo tarehe 30 mwezi Oktoba mwaka huu mradi huu utakabidhiwa rasmi na kuanza kutumika kwani hadi sasa umefikia asilimia 96 ya ujenzi na unatarajiwa kuboresha huduma hii muhimu kwani utaunganishwa kwenye mtandao wa mabomba ya zamani na mtandao mpya."Amesisitiza Bi. Nelly.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.