RC MTANDA AMSHUKURU RAIS SAMIA KWA KUIDHINISHA BILIONI 19 KUTEKELEZA MRADI WA UMEME VITONGOJINI MWANZA
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa zaidi ya Bilioni 19 kwa ajili ya kutekeleza mradi wa umeme kwenye vitongoji 135 Mkoani humo katika majimbo yote tisa.
RC Mtanda ametoa pongezi hizo leo Septemba 12, 2024 Ofisini kwake wakati akizungumza na ujumbe wa wakala wa nishati vijijini (REA) uliomtembelea wakiongozana na Cylex Engineering Company ambaye ndie mkandarasi wa mradi huo.
Amesema Mhe. Rais anaendelea kuboresha maisha ya wananchi wake kwa kasi ndio maana amemaliza kuweka huduma za umeme kwenye vijiji vyote nchini na sasa anaelekeza nguvu kwenye vitongoji kwa kuhakikisha wanapata nishati hiyo muhimu.
Aidha Mkuu wa Mkoa ametoa wito kwa wakala kumsimamia mkandarasi vema ili akamilishe mradi kwa wakati na kwa mujibu wa mkataba ili haraka iwezekanavyo huduma za umeme ziweze kuwafikia wananchi.
Vilevile, amemtaka mkandarasi huyo kuwatumia wananchi wazawa kwenye maeneo ya mradi katika ajira ndogondogo zitakazotolewa na kuhakikisha wanawalipa kwa wakati ili kuepusha migogoro isiyo lazima kwenye eneo la kazi.
Akizungumzia upatikanaji wa huduma ya umeme Mhe. Mtanda amesema Mwanza ina nishati ya kutosha kwani ni megawati 86 pekee zinatumika kwa sasa pamoja na kuzalishwa zaidi ya megawati 100 hivyo kumekua na ziada ambayo itatumika pindi miradi ya kimkakati itakapoanza.
Awali, msimamizi wa miradi ya Wakala wa Nishati vijijini (REA) Kanda ya Ziwa Mhandisi Ernest Makale amesema mradi huo kwenye vitongoji unadhihirisha na kubainisha nia ya Serikali ya kuhakikisha kila kijiji na kitongoji nchini kinakua na umeme ifikapo 2030.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.