RC MTANDA AMTAKA MKANDARASI BARABARA YA FORTES KUKAMILISHA UJENZI MARA MOJA
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda amemtaka Mkandarasi anayejenga barabara ya Fortes iliyopo kwenye mtaa wa kaskazini B Isamilo kwa kiwango cha zege kwa Tshs. Milioni 87.3 fedha kutoka Tozo za Mafuta (Usimamizi wa TARURA) kukamilisha ujenzi haraka ili kurahisisha usafiri kwa wananchi waishio milimani.
Mhe. Mtanda ametoa agizo hilo kwa Mkandarasi M/s Polas Group companies limited leo Julai 17, 2024 akiwa kwenye ziara ya ukaguzi wa barabara hiyo iliyopo kwenye mtaa wa kaskazini B kata ya Isamilo iliyokamilika kwa asilimia 90 huku ikitarajiwa kukamilika tarehe 20 Oktoba 2024 kwa mujibu wa mkataba.
Sambamba na hilo, Mhe. Mtanda amemuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza kutenga fedha haraka kwa mwaka 2024/25 ili kushirikiana na TARURA kukamilisha ujenzi wa kipande kilichobaki kitakachotokezea mtaa wa Pepsi ili kuongeza kasi ya ukuaji wa Jiji hilo.
Naye Meneja Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (TARURA) wilaya ya Nyamagana Mhandisi Danstan Kishaka amebainisha kuwa mradi huo ulioanza Aprili mwaka huu utasaidia pia kuvutia biashara na uwekezaji na kwamba kazi zilizotekelezwa ni pamoja na ujenzi wa barabara, mitaro mita 34 pamoja na ujenzi wa ukuta wa mawe (Stony Masonry)Mita 120.
Vilevile, Mhe. Mkuu wa Mkoa amewaelekeza TARURA kuweka matoleo ya Barabara inayounganisha mtaa huo kwenda mji mwema ili kulinda eneo hilo lisivamiwe na kusababisha mgogoro wa ardhi kwani kwa sasa hakuna alama ya kwamba panatakiwa kuunganishwa barabara hiyo kama ambavyo inakusudiwa.
Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Isamilo, Mhe. Charles Nyamasilili ametumia wasaa huo kuwashukuru TARURA kwa kuwaondolea changamoto ya barabara wananchi wanaoishi kwenye miinuko na amempongeza Mhe. Rais Dkt. Samia kwa kuelekeza fedha kwenye miradi.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.