Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda leo tarehe 21 Septemba, 2025 ameshuhudia jaribio la mwisho la safari ndefu kwa Meli ya MV New Mwanza kwenye bandari ya Mwanza Kusini iliyopo jijini Mwanza ilipoondoka kuelekea kwenye Bandari ya Bukoba (Neutical Miles 100).
Akizungumza na wananchi waliojitokeza kushuhudia hafla hiyo ya kihistoria Mhe. Mtanda amesema kukamilika kwa meli hiyo ni ishara ya juhudi za serikali katika kuimarisha sekta ya usafiri na usafirishaji wa abiria na mizigo katika ukanda wa ziwa Victoria.
Aidha, amesema wananchi wa Mwanza na ukanda wa ziwa Victoria kwa ujumla wamepata usafiri wa uhakika kwani Mhe. Rais Samia amedhamiria kuwaondoka kwenye adha ya ajali zilizotokana na matumizi ya usafiri duni wa mitumbwi na kwamba nauli zitakua nafuu sana kwa safari za ndani na nje ya nchi.
Ameongeza kuwa katika kuhakikisha katika ukanda huo kunakua na usalama katika usafiri, usafirishaji na hata uvuvi serikali kwa kushirikiana na nchi wanachama wa Jumuiya Afrika Mashariki wanajenga kituo maalum cha uokozi katika eneo la Malaika Beach kwa gharama ya zaidi ya Bilioni 5.
Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Meli nchini (TASHICO) Bw. Eric Hamissi amebainisha kuwa Ujenzi wa meli hiyo umefikia asilimia 99 na baada ya safari hiyo ya Mwanza- Kemondo hadi Bukoba wanatarajia kupata majibu ya ufanisi wake kitaalamu na mara moja kuanza safari katika Ziwa Victoria.
Amesema, pamoja na changamoto kama za kupanda kwa gharama za vifaa kama vya vyuma na wataalamu kushindwa kufika kwa wakati hatimaye meli hiyo ya kisasa yenye urefu wa mita 92.6 yenye spidi kubwa leo hii imekamilika na itafika Bandari ya Bukoba kwa saa 6 pekee.
Aidha, amebainisha kuwa meli hiyo yenye uzito wa tani elfu nne (4000) na ghorofa nne, ina uwezo wa kubeba abiria 1200, Magari 20 madogo, Malori 3 imejengwa na watanzania zaidi ya 200 walioshirikiana na timu ya wataalamu 16 tu wa mkandarasi kutokea nchini Korea Kusini.
"Kwa mara ya kwanza Meli hii itafika katika bandari ya Bukoba na italala huko na kesho itarejea Mwanza na imejengwa kwa zaidi ya Tshs. Bilioni 120 ambapo ni lazima tumshukuru Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwani ameikuta kwenye 40% tu ya ujenzi mwaka 2021 huku zikiwa zimelipwa Tshs. Bilioni 36 pekee lakini amemalizia fedha zote." Amebainisha Mkurugenzi.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.