Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda amepokea rasmi utambulisho wa wakandarasi wapya wa kupeleka umeme kwenye vitongoji mbalimbali vya Mkoa wa Mwanza chini ya Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kwa kipindi cha miaka mitatu.

Wakandarasi hao ni White City International Contractors Ltd na Tibea Company Ltd, ambao wamesaini mikataba miwili ya utekelezaji wa mradi huo mkubwa unaolenga kusogeza huduma ya umeme kwa wananchi wa vijijini na maeneo ya pembezoni.

Akizungumza wakati wa utambulisho huo, Mhe. Mtanda amewataka wakandarasi hao kufanya kazi kwa weledi, uaminifu na kuzingatia maadili ya kazi ili kufanikisha malengo ya Serikali ya kuwahudumia wananchi kwa haki na usawa.

Amesema Ofisi yake itafanya ukaguzi wa mara kwa mara kufuatilia utekelezaji wa mradi huo, huku akisisitiza kuepuka vitendo vya rushwa wakati wa kuwaunganisha wananchi na huduma ya umeme.

Mhe. Mtanda pia ametoa wito kwa wananchi kuwapokea vizuri wakandarasi hao na kuhakikisha wanapitia ngazi zote za Uongozi kuanzia Wilaya, Kata, Kijiji hadi Kitongoji ili kuwaelezea Viongozi kwa kina kuhusu mradi huo na vigezo vya uunganishaji.

Ameeleza kuwa nia ya Serikali ni kusogeza huduma karibu na wananchi, na pale mahitaji yatakapoongezeka, maboresho yatafanyika ili kuongeza upatikanaji wa umeme kwa wananchi wengi zaidi.

Kwa upande wake, Kaimu Meneja wa Miradi kutoka Ofisi ya Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Seif Abdallah amesema Mkoa wa Mwanza umesaini jumla ya kandarasi mbili kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo.

Amesema mradi huo utatekelezwa katika vitongoji 619 vya wilaya tano za Mkoa wa Mwanza kwa gharama ya shilingi bilioni 66.7 na unatarajiwa kuwanufaisha wateja 19,878.

Amefafanua kuwa White City International Contractors Ltd itahudumia vitongoji 306 katika Wilaya za Misungwi na Magu kwa gharama ya shilingi bilioni 32.7, huku Tibea Company Ltd ikitekeleza mradi katika vitongoji 313 vya Wilaya za Kwimba na Sengerema kwa gharama ya shilingi bilioni 33.7.

Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.