Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda amewataka wananchi wa mkoa huo kuchangamkia fursa ya Bima ya Afya kwa Wote kwa kuunda kaya za watu sita ili kunufaika na huduma hiyo. Amewahimiza hata wanawake wasio na waume (wasimbe) na wanaume wasio na wake (wabanza) kuungana na kuunda kaya zitakazowawezesha kukata bima.

Mtanda amesema lengo ni kuondoa hofu kwa watu wasio na familia au waliotengana na wenza wao, kuwa nao wanaweza kujiunga kwa kushirikiana na wengine. Amesisitiza kuwa mpango huo ni wa wote na unalenga kuhakikisha hakuna mwananchi anayekosa huduma za afya kwa sababu ya ukosefu wa kaya rasmi.

Akizungumza katika Kijiji cha Mwanekeyi, Kata ya Matare, Wilaya ya Kwimba wakati wa uzinduzi wa Shule ya Msingi Mwanekeyi, RC Mtanda pia amewataka wazazi kuhakikisha wanawapeleka watoto wote wanaostahili kujiunga na elimu ya awali, msingi na kidato cha kwanza.

Amesema hadi sasa wanafunzi 6,622 wa kidato cha kwanza wameripoti shule Wilayani Kwimba, huku 1,587 bado hawajaripoti. Amewaagiza Mkuu wa Wilaya, Kamati ya Usalama, Mkurugenzi na Maafisa Elimu kutembea nyumba kwa nyumba kuwatafuta watoto hao na kuwapeleka shule haraka.

Aidha, amesisitiza kuwa hakuna mwanafunzi anayepaswa kurudishwa nyumbani kwa kukosa sare, viatu au michango. Ameagiza watoto wapokelewe kama walivyo huku wazazi wakipewa muda wa kukamilisha mahitaji hayo, akionya kuwa kutotekeleza agizo hilo ni ukaidi.

RC Mtanda pia amewataka walimu na wanafunzi kuitunza miundombinu ya shule ili idumu kwa muda mrefu. Mradi wa ujenzi wa shule hiyo ulitekelezwa kwa siku 90 kuanzia Novemba 13, 2025 hadi Februari 9, 2026 kwa gharama ya Sh.330,700,000, ambapo Sh.300,684,969.06 zimetumika na Sh.30,015,030.94 zinaendelea kutumika kukamilisha kazi zilizobaki.

Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.