Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda amezindua Shule ya Msingi Kanyerere iliyopo Kata ya Mkuyuni jijini Mwanza na kuishukuru Serikali Kuu kwa kutoa zaidi ya Sh370 milioni kukamilisha ujenzi huo.

Amepongeza wananchi kwa kuchangia ardhi, nguvu kazi na zaidi ya Sh17.5 milioni kufanikisha mradi huo na wadau zaidi ya milioni 35. Mradi huo uliotekelezwa kwa mfumo wa Force Account umegharimu jumla ya Sh424,856,500 na umehusisha ujenzi wa madarasa 13, ofisi tatu, jengo la utawala na matundu 10 ya vyoo. Fedha zimetoka Halmashauri ya Jiji la Mwanza, wananchi na wadau mbalimbali.

Shule ilianza kujengwa Desemba 2023 na kuanza kutumika Novemba 2025. Kwa sasa ina wanafunzi zaidi ya 1,000 kati yao 808 waliohamishwa kutoka Shule ya Msingi Tambukareli (wavulana 375 na wasichana 433), hatua iliyopunguza msongamano wa wanafunzi.

Akijibu ombi la Diwani wa Butimba kuhusu ujenzi wa chumba cha wagonjwa maalum katika Hospitali ya Wilaya ya Nyamagana, amesema atashirikiana na Mbunge kuhakikisha hospitali hiyo inasimamiwa ipasavyo.

Kuhusu barabara ya Mkuyuni–Nile Peach yenye urefu wa kilomita 10.5 na gharama ya zaidi ya Sh22 bilioni, amesema wamekubaliana na TARURA kuanza na kilomita tano huku akiahidi kuwasiliana na Mtendaji Mkuu wa TARURA ili ujenzi uanze kwani upembuzi yakinifu tayari umekamilika.

Sambamba na hayo Mkuu wa Mkoa ameahidi kuunga mkono juhudi za wananchi na wadau katika ujenzi wa Ofisi ya Serikali ya Mtaa huo atachangia mifuko 50 ya saruji na matofali 1000.

Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.