SERIKALI KUJENGA HOSPITALI YENYE HADHI YA MKOA WILAYANI UKEREWE
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda amemshukuru Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa uboreshaji wa sekta ya afya mkoani humo hususani ujenzi wa miundombinu bora na ufungaji wa vifaa vya kisasa katika vituo vya kutolea huduma.
Mhe. Mtanda amebainisha hayo leo tarehe 27 Desemba, 2024 katika hafla ya utiaji saini mkataba wa ujenzi wa Hospitali ya Rufaa yenye hadhi ya Mkoa itakayojengwa katika kijiji cha Bulamba kata ya Bukindo kwa thamani ya zaidi ya Bilioni 25.
Ameongeza kuwa ndani ya muda mfupi Serikali imepeleka Mkoani humo zaidi ya Tshs. Bilioni 49.4 kwa ajili ya uboreshaji wa huduma za afya na jumla ya Trilioni 5.6 zimepokelewa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi katika sekta mbalimbali.
Aidha, amemtaka mkandarasi pamoja na msimamizi yaani Ofisi ya Mkuu wa Mkoa kutekeleza mradi huo kwa wakati kwa mujibu wa mkataba na kwa kuzingatia ubora na amewataka kuanza mara moja ujenzi kwakua tayari Bilioni 6 zimeshatolewa na Serikali.
"Uwepo wa Ujenzi huu utawafanya wananchi wa eneo hili na maeneo ya jirani kukua kiuchumi kutokana na kuongezeka kwa muingiliano wa watu na kufungua fursa kwa sekta zingine kwa kuwekeza jirani na eneo hili, hivyo tunamshukuru sana Mhe. Rais kwa upendo huu." Amesisitiza.
Akielezea mradi huo utakaotekelezwa na kampuni ya M/S DIMETOCLASA REALHOPE LIMITED kwa kipindi cha miezi 18, Katibu Tawala Msaidizi sehemu ya Miundombinu Mkoa wa Mwanza Mhandisi Chagu Ng'oma amesema mradi huo umegawanywa katika awamu 4.
Aidha, ameahidi kusimamia kwa dhati utekelezaji wa mradi huo ambao amefafanua kuwa awamu ya kwanza utahusisha ujenzi wa jengo kuu la hospitali litakalokuwa na uwezo wa kubeba vitanda 180, Ofisi tatu za walinzi, Jengo la kuhifadhia maiti na Jengo la umeme na kazi za nje.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.