Maadhimisho ya Siku ya Sheria Nchini (Law Day) 2026 Kimkoa yamefanyika katika Kiwanja cha Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Buswelu, Wilaya ya Ilemela, yakilenga kuangazia mchango wa Mahakama katika ustawi wa jamii na maendeleo ya Taifa.

Akizungumza katika maadhimisho hayo, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda amesema Serikali itaendelea kushirikiana na mhimili wa Mahakama kwa kuwa ni mdau muhimu katika kusimamia haki na kuhakikisha wananchi wanapata haki kwa wakati.

Mhe. Mtanda amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kuwekeza katika ujenzi wa Mahakama na kuimarisha upatikanaji wa haki kupitia kampeni ya Mama Samia Legal Aid.

Amesema kupitia kampeni hiyo, mashtaka 1,572 yamesikilizwa, kesi 580 zimekamilika huku kesi 992 zikiendelea kufanyiwa kazi, pamoja na kutolewa elimu ya sheria na huduma za utatuzi wa migogoro.

Mhe. Mtanda amesema katika kupunguza mlundikano wa mashauri Mahakamani, Serikali imekuwa ikitatua kero kuanzia ngazi za chini kabla hazijageuzwa kuwa mashauri ya Mahakama.

“Kwa Mkoa wa Mwanza, jumla ya kero 249 zimesikilizwa ambapo 213 zimekamilika na 36 zinaendelea kufanyiwa kazi”.

Kwa upande wake, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Mwanza, Mhe. Dkt. Ntemi Kilekamajenga amesema Siku ya Sheria ni fursa ya kujitathmini endapo haki imetendeka na kuonekana kwa wananchi.

Amebainisha kuwa Mahakama ni mlinzi wa Katiba, mlezi wa haki za raia na ngome ya wanyonge, sambamba na kusukuma maendeleo ya Taifa kupitia amani na utulivu.

Amesema kuanzia Januari hadi Desemba 2025, kesi 15,105 zilifunguliwa katika Mahakama za Kanda ya Mwanza, kesi 18,236 zikaamuliwa huku kesi 4,086 zikiendelea.

Naye Wakili wa Serikali kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mkoa wa Mwanza, Bw. Kabyemela S. Lushagara amesema Siku ya Sheria ni kioo cha kutafakari wajibu wa Sheria na Mahakama katika kulinda haki, amani na usawa.

Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.