SHEREHE ZA BULABO KUPANDISHWA HADHI KUWA URITHI WA UTAMADUNI
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Chifu Mkuu Hangaya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema kuwa serikali imeamua kuboresha tamasha la Bulabo kuwa la Urithi wa Utamaduni usioshikika na kwamba Wizara ya Utamaduni inakamilisha taratibu ili kufikia malengo hayo.
Mhe. Dkt. Samia ameeeleza hayo leo tarehe 21 Juni, 2025 wakati akifungua tamasha la utamaduni wa Wasukuma (Bulabo) la kanda ya ziwa lililofanyika katika Viwanja vya Red Cross Bujora – Kisesa wilayani Magu na amesisitiza jamii kuenzi na kulinda utamaduni kwa maslahi ya sasa na vizazi vijavyo.
“Hakika nimeshuhudia mambo mazuri sana ya kihistoria, hongera kwa kujenga taifa lenye maadili nawapongeza sana kwa kudumisha utamaduni lakini niendelee kusisitiza kulinda kikamilifu silka na mila zetu na tuache kuiga mila za kigeni zinazoweza kuharibu amani yetu.” Dkt. Samia.
Aidha, kuelekea kipindi cha uchaguzi amewataka waganga kutofanya ramli chonganishi kwa wagombea wa nafasi mbalimbali za uongozi nchini ili kuendelea kulinda uhai na utu wa watu wa makundi yote.
Kwa upande wake Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Prof. Palamagamba Kabudi amesema serikali imejiridhisha na uendeshaji wa sherehe za mavuno ya bulabo zinazotunza mila zikiwa zimeunganishwa na Ekaristi Takatifu ya Kanisa Katoriki ambapo Wizara ipo katika hatua za mwisho kulifanya Tamasha hilo kuwa Urithi wa Utamaduni usioshikika wa dunia chini ya UNESCO.
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda amesema tamasha hilo limelenga kuhamasisha utunzaji wa mazingira, kulinda tamaduni na wananchi kushiriki uchaguzi Mkuu wa 2025 na kwamba Mwanza kuna wapiga kura wapya zaidi ya laki tano kutoka kwenye waliopiga kwenye uchaguzi uliopita Milioni 1.8.
Naye Baba Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoriki la Mwanza, Mhashamu Renatus Nkwande amemshukuru Rais Samia kwa kutambua nafasi ya utamaduni na kuruhusu utoaji wa vibali kwa ajili ya kumiliki nyala za serikali katika kituo cha Bujora ili kukipatia uhai na kuleta taswira halisi.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.