UANDIKISHAJI UCHAGUZI SERIKALI ZA MITAA WAFIKIA 45% NCHINI - WAZIRI MCHENGERWA
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mhe. Mohamed Mchengerwa amewataka wananchi kuendelea kujiandikisha kwenye daftari la wapiga kura ili waweze kushiriki uchaguzi wa serikali za mitaa Novemba 27, 2024.
Amesema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari leo Oktoba 15, 2024 katika ukumbi wa Halmashauri ya jiji la Mwanza kwa lengo la kufikisha elimu na hamasa kwa Wananchi juu ya umuhimu wa kujiandikisha.
Mhe. Mchengerwa amewataka wananchi wenye sifa na wanaokidhi vigezo vya kugombea wajitokeze kuchukua fomu kuanzia Oktoba 26, 2024 mpaka Novemba 1, 2024 ili waweze kugombea nafasi mbalimbali za uongozi wa serikali za Mitaa na Vijiji.
Vilele Waziri Mchengerwa amewataka wasimamizi wa uchaguzi kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia Sheria, kanuni, miongozo pamoja na maelekezo ya usimamizi wa uchaguzi.
"Maelekezo yangu kwa wasimamizi wa uchaguzi kuzingatia kanuni viapo na kutekeleza majukumu kwa mujibu wa viapo vyao". Amesisitiza Mhe. Mchengerwa.
Aidha Mhe. Mchengerwa amewataka Viongozi wa vyama mbalimbali vya siasa kutoa elimu kwa wanachama wao juu ya kujiandikisha na kushiriki uchaguzi wa Serikali za mitaa.
Zoezi la kujiandikisha katika daftari la makazi limeanza rasmi Oktoba 11, 2024 mpaka Oktoba 20, 2024 ambapo kila Mwananchi mwenye sifa na vigezo anatakiwa kujiandikisha katika eneo analoishi ili aweze kushiriki zoezi la Uchaguzi wa Serikali za mitaa.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.