WAFUGAJI MWANZA WATAKIWA KUFUGA KISASA KUKIDHI MAHITAJI SOKO LA NYAMA KIMATAIFA
Mkuu wa mkoa Mwanza Mhe. Said Mtanda amewataka wafugaji Mkoani humo kuachana na ufugaji wa kienyeji wa mazoea na kufuga kisasa mifugo yao ili wakidhi mahitaji ya soko la nyama kimataifa.
Mhe. Mtanda ametoa wito huo leo Septemba 2.2024 alipotembelea kiwanda cha nyama cha Chobo Investment kilichopo wilayani Misungwi kujionea uzalishaji na uchakataji nyama unaofanywa na kiwanda hicho.
Amesema nchi yetu ina zaidi ya ng'ombe Milioni 40 na inashika nafasi ya pili kwa ufugaji ng'ombe ikitanguliwa na Ethiopia lakini ni asilimia 5 tu ya mifugo hiyo ndio wanafaa kwa uzalishaji nyama hiyo, hali inayopelekea pia kutokufanya vizuri katika uchangiaji wa pato la Taifa ambapo kwa sasa ufugaji unachangia kwa asilimia 7 tu.
Aidha, amempongeza mwekezaji huyo kwa kupanua kiwanda hicho kwa dola za kimarekani milioni 3 zaidi kutoka kwenye 10 za awali zilizolenga kuongeza uchakataji wa mazao ya nyama kutoka matumizi ya 47% hadi 100% na kwamba itasaidia pia kupatikana kwa bidhaa 153 zinazotokana na mfugo ng'ombe.
Naye, Mkurugenzi wa kiwanda hicho Bw. John Chobo amesema kiwanda chao kina uwezo wa kuchinja ng'ombe 600 kwa saa 8 lakini kwa sasa wanachinja 200 tu huku wakipata mbuzi wachache kutokana na uzalishaji kuwa wa kiwango cha chini na usiokidhi mahitaji.
Amefafanua kuwa ili kufikia malengo ya kupata nyama ya kutosha wameanzisha shamba ambalo wanafuga kisasa, wananenepesha na kuandaa malisho bora kwa mifugo na akatumia wasaa huo kuwakaribisha wafugaji kwenda kujifunza ili wazalishe kisasa.
"Kiwanda chetu ni kikubwa na tumekiongezea nguvu hivyo tunatamani kupata ng'ombe wenye uzito mkubwa hadi wa Kilogram 700 kwani mahitaji ya nyama kwenye soko la ndani na nje ni makubwa sana lakini kunakua na uhaba kutokana na ng'ombe wa asili kuwa na uzito mdogo." Amesema Bwana Chobo.
Vilevile, ametoa wito kwa sekta ya kilimo kuchangia kwenye ukuaji wa nyama kwa kuzalisha vifungashio vitokanavyo na zao la pamba linalofanya vizuri nchini (Mutton Cloth) vinavyotumika kuhifadhi nyama kwenda nje ya nchi tofauti na hali ya sasa ambapo vinaagizwa kutoka Vietnam.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.