WAKAZI 3147 KIJIJI CHA MHULYA KWIMBA WANUFAIKA NA MRADI WA MAJI
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuongeza upatikanaji wa maji safi na salama kwa wananchi wa kijiji cha Mhulya kutoka 40% hadi 90% kutokana na kuwajengea mradi wa maji wenye thamani ya Tshs. 667.1 milioni fedha za mfuko wa maji wa Taifa na PforH.
Mhe. Mtanda ametoa shukrani hizo leo tarehe 14, 2024 katika Kijiji cha Mhulya kilichopo Kata ya Ngula Wilayani Kwimba wakati akikagua mradi wa maji kutoka kwenye chanzo cha kisima kirefu cha mita 80 chenye uwezo wa kuzalisha maji lita 12,336 kwa saa ambao umekamilika tangu mwezi juni 2023 chini ya usimamizi wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA).
Aidha, Mhe. Mtanda amewataka wananchi kulinda miundombinu ya mradi huo na viongozi wanaosimamia jumuia ya watumia maji kuketi na wananchi na kukubaliana nao juu ya bei ya kuuziana maji kwenye mradi huo.
"mnaweza mkaamua kama uchangiaji wa huduma na fedha zinazopatikana zitumike kufanya ukarabati na marekebisho ya miundombinu itakapohitajika". Ameongeza Mhe. Mtanda.
Vilevile, Mkuu wa Mkoa amewahamasisha wananchi hao kujiandikisha kwenye orodha ya daftari la wapiga kura na kushiriki katika uchaguzi wa serikali za mitaa utakaofanyika novemba 27.
Naye Meneja wa RUWASA Wilaya ya Kwimba Mhandisi Godliva Gwambasa amesema mkandarasi KPR ameshakamilisha kazi na maji yanatoka kwenye vituo vyote 9 vya kutolea maji kwenye kijiji hicho na mradi huo kwa sasa unaendeshwa na wananchi wenyewe chini ya chombo cha kuendeshea maji (CBWSO) cha kijijini hapo.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.