Serikali kwa kushirikiana na Benki ya Uwekezaji ya Ulaya wanatekeleza Ujenzi wa Mfumo rahisi wa Maji taka kwenye makazi ya miinuko unaotekelezwa Tshs Bilioni 3.8 unaosaidia kuhifadhi maji taka kwenye matanki maalum na kuyatibu badala ya kumwaga kwenye ziwa Victoria kama ilivyokua awali.
Hayo yamebainika leo Juni 07, 2022 mtaa wa Igogo -Sahara wakati wa ziara ya Mhe Mhandisi Robert Gabriel, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza akiambatana na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa alipokua akikagua Miradi ya Maendeleo wilayani Nyamaga pamoja na kusikiliza na kutatua kero za wananchi.
Vilevile, kupitia mradi huo kaya 122 zimeundiwa mfumo wa maji safi na umewezesha ujenzi wa njia maalum za kupanda na kushuka kwenye mitaa hiyo ambapo baada ya ukaguzi wake Mhe Mkuu wa Mkoa ameridhishwa na mradi huo na amewapongeza watekelezaji wa mradi huo wa kisasa wenye ubunifu.
Vilevile, Mhe Mkuu wa Mkoa ametoa wito kwa Maafisa Maendeleo ya Jamii kutoka Halmashauri ya Jiji la Mwanza kutoa elimu ya biashara kwenye vikundi vyote wanavyowakopesha fedha kutoka makundi ya Wanawake, Vijana na wenye ulemavu kwenye Halmashauri hiyo ili kuweka uhai wa vikundi wanavyokopeshwa.
Mkuu wa Mkoa ametoa wito huo kwenye Mradi wa kikundi cha Vijana watano cha Yuoth Box Media kilichokopeshwa Tshs Milioni 49 mwaka 2021 ambacho kwa sasa kimekuza mtaji hadi kufikia thamani ya Tshs. Milioni 81 huku kikimiliki bidhaa za Habari kupitia Chaneli za mtandaoni za Yu box Tv na Yu box Studio.
"Hawa wanafanya vizuri ila mimi nimekuja kuona kama kikundi kina afya, je wana taarifa za mapato na matumizi ya kikundi, wana vitabu vya fedha na wana utaratibu wa kupima maendeleo ya kikundi chao, hapo lazima tujiulize na Maafisa Maendeleo hiyo ndio kazi yetu kuwajengea uwezo", amesema.
Aidha, Mhe. Mkuu wa Mkoa amekagua Ujenzi wa Barabara ya Hesawa-Yatch Makaburini, Tilapia -Vickfish yenye urefu wa Mita 650 liyotekelezwa kwa zidi ya Tshs. Milioni 348 na ameagiza kurekebisha dosari ndogo kwenye kingo za barabara hizo na kusafisha mazingira.
Akiendelea na ziara yake Mhe Mkuu wa Mkoa ametoa pongezi kwa ujenzi wa Mradi wa vyumba 06 vya madarasa kwa mfumo wa ghorofa katika shule ya Sekondari Mkuyuni unaotekelezwa kwa Tshs. Milioni 310 utakaosaidia kupunguza msongamano wa wanafunzi kutoka 85 hadi 52 kwa darasa kwani madarasa hayo yatachukua wanafunzi 900.
Baada ya kukagua uhai wa Vilabu vya kupambana na rushwa na dawa ya kulevya katika shule ya msingi Nyegezi msafara wa Mhe Mkuu wa Mkoa ulifika kwenye Mradi wa Anuani za Makazi katika Mtaa wa Kisese kata ya Mkolani.
Kabla ya kukagua ujenzi wa jengo la Benki ya CRDB tawi la Buhongwa wenye thamani ya Tshs. Milioni 500, Ujenzi wa Kituo cha Afya Bulale kata ya Buhongwa wenye thamani ya Tshs Milioni 500 umehitimisha ukaguzi wa miradi wilayani Nyamagana ambapo Mhe. Mkuu wa Mkoa amesisitiza ukamilishaji wa mradi huo kwa wakati ili uanze kuwahudumia zaidi ya wananchi elfu 5 wanaokusudiwa.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.