WASIOFANYA MAZOEZI HATARINI KUPATA MAGONJWA YASIYOAMBUKIZA
Mganga Mkuu Mkoa wa Mwanza Dkt. Jesca Lebba amewasisitiza Watumishi wa umma na Wananchi kuzingatia ufanyaji mazoezi kwa kuwa magonjwa yasiyo ya kuambikiza yanaongezeka kwa kasi hivyo njia pekee ya kuepuka hatari hiyo ni kufanya mazoezi.
Dkt. Lebba ameyasema hayo asubuhi ya leo tarehe 22 Februari, 2025 alipokuwa akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza mara baada ya kuhitimisha matembezi ya kuzuia magonjwa yasiyo ambukiza kwa watumishi na Wananchi.
Mganga Mkuu amesema kwa Mkoa wa Mwanza mwaka 2020 magonjwa yasiyo ya kuambukiza yalikuwa yanachangia kwa 6% na mwaka jana tumefika 8% hivyo yanakwenda yanaongezeka kwa kasi na kusisitiza kuzingatia kufanya mazoezi.
“Hata hapa ofisini asilimia zaidi ya 90 wana viashiria vya magonjwa yasiyo ya kuambukiza kwa hiyo wote tuko katika hatari na mazoezi yanasaidia vitu vingi sana”. Amesema.
Aidha, ameongeza kuwa magonjwa hayo yasiyo ya kuambiza kama vile kisukari, saratani, changamoto mbalimbali za figo, magonjwa ya moyo, yote hayo yana gharama kubwa sana na yana zuilika kwa mazoezi na kubadilisha mtindo wa maisha.
“Magonjwa haya zamani tulizoea kuyaona kwa matajiri lakini sasa hata kwa maskini lakini pia tulizoea kuona kwa wenye umri mkubwa lakini kwa sasa hata chini ya miaka 30”. Amesisitiza Mganga Mkuu.
“...kwa hiyo wote tuko katika hatari, tuendelee kushiriki mazoezi na niwahamasishe kujitokeza kwa wingi kufanya mazoezi.” Ameongeza Mganga Mkuu.
Matembezi hayo maalumu ya kuzuia magonjwa yasiyo ambukiza kwa watumishi na Wananchi yanalenga kuimarisha afya, yalizinduliwa rasmi Januari 18, 2025 hivyo leo ni mwendelezo na hufanyika kila jumamosi ya tatu ya mwezi.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.