WATOA HUDUMA ZA TIBA ASILI NA TIBA MABADALA WATAKIWA KUKEMEA VITENDO VYA UKATILI.
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda amewataka watoa huduma za afya kwa njia ya tiba asili na tiba mbadala kuhakikisha wanashirikiana na serikali katika kukemea na kuzuia vitendo vyote vya kikatili ikiwemo mauaji ya watoto na wenye ulemavu wa ngozi.
Wito huo umetolewa leo Agosti 28 wakati akifungua maadhimisho ya siku ya tiba asili ya Mwafrika yanayoendelea katika viwanja vya Furahisha Manispaa ya Ilemela.
Aidha Mhe. Mtanda Amesema waganga wa tiba asili wote wanatakiwa kujisajili kwenye baraza la tiba asili na mbadala na kuhusisha leseni zao kila mwaka ambapo kwa kufanya hivyo watakuwa wakikumbwa na sheria na taratibu za utoaji huduma hizo nchini
"Mimi ninaamini tiba hizi za asili zinapoboreshwa zinafanya kazi sawa na tiba hizi za kawaida na ndio maana Watanzania zaidi ya asilimia 60 nchini wanatumia tiba hizi na zinawasaidia".
Wote tunatambua kwamba tiba asili na tiba mbadala zimekuwa na mchango mkubwa kwa wananchi na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa kupitia seksheni ya afya itatoa ushirikiano mkubwa ili kuhakikisha jamii inapata huduma bora". Ameongeza Mhe. mtanda
Naye Makamu Mwenyekiti wa Baraza la tiba asili na mbadala Dkt. Elizabeth Lema amesema waganga wa tiba hizo wametoka kwenye mfumo wa kufanya kienyeji na sasa wanafanya kisasa na wakati mwingine wanatoa huduma jumuishi na wataalamu kutoka hospitali za kawaida ambao wanakiri kwamba tiba za asili zinamsaada mkubwa katika kutibu magonjwa mbalimbali.
Aidha kwa upande wake Kaimu Msajili Baraza la tiba asili na mbadala Bw. Martin Mgogwa amebainisha kuwa baraza hilo pamoja na kuwasajili linasimamia, kuthibiti na kuendeleza tiba asili nchini kwa kuhakikisha kila anayetoa huduma za tiba asili anasajiliwa pamoja na kuhuisha leseni kila mwaka katika eneo lake.
Naye, Meneja wa Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali wa Kanda ya Ziwa Bw. John Wanjala ametoa wito kwa wadau kuhakikisha wanafika kwenye ofisi hizo ili dawa wanazotumia ziweze kuchunguzwa kama zina kemikali dawa badala ya kuwa na sumu.
Maadhimisho hayo ya siku ya tiba asili ya Mwafrika yaliyoanza tangu Agosti 25 mpaka Agosti 31 yanalengo la kusimamia utoaji huduma bora na salama za tiba asili kupitia mifumo sahihi ya udhibiti.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.