Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba (MB) anatarajiwa kuzindua Meli ya kisasa ya MV. New Mwanza katika Bandari ya Mwanza Kusini kesho ijumaa tarehe 23 Januari, 2026.

Hayo yamebainishwa na Mhe. Prof. Makame Mbarawa (MB), Waziri wa Uchukuzi leo tarehe 22 Januari, 2026 wakati akizungumza na Waandishi wa Habari katika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza.

Prof. Mbarawa amesema Meli ya MV Mwanza imejengwa na Mkandarasi Gas Entec Ship- Building kutoka Korea kwa kushirikiana na Kampuni ya Meli nchini (TASHICO) kwa gharama ya Tshs. Bilioni 120.56.

Amefafanua kuwa Ujenzi wa Meli hiyo umezingatia teknolojia ya juu na kwamba mpaka sasa meli hiyo imefanyiwa safari sita za majaribio (Mwanza - Bukoba) kuanzia mwezi Machi 2025 ambapo majaribio hayo yameonesha ufanisi mkubwa na TASAC imeridhika na ubora na kuruhusu kuanza kwa safari.

Aidha, ameongeza kuwa Meli hiyo ya ghorofa 4 ndiyo kubwa zaidi ya zote ndani ya ukanda wa maziwa makuu na ina uwezo wa kubeba abiria 1200, tani 400 za mizigo, magari madogo 20 pamoja na makubwa 3 kwa wakati mmoja.

Naye, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda ametumia wasaa huo kuwakaribisha wananchi wa Mkoa huo pamoja na mikoa ya jirani kumlaki na kushiriki kwenye ziara hiyo ya kitaifa ya Mhe. Waziri Mkuu kuanzia saa 2 asubuhi.

Mhe. Mtanda amebainisha kabla ya Mhe. Waziri Mkuu kuzindua mradi huo ataanza na Ukaguzi wa mradi wa Ujenzi wa kituo cha kuratibu ufuatiliaji na uokozi katika ukanda wa ziwa Victoria katika eneo la Uwanja wa Ndege wa Mwanza wilayani Ilemela.

Ameongeza kuwa baada ya hapo Mhe. Waziri Mkuu ataweka pia jiwe la Msingi katika Mradi wa Ujenzi wa Matenki, Vituo vya Kusukuma Maji na Mabomba Makuu katika Mtaa wa Sahwa kata ya Lwahnima Jijini Mwanza.

Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.