Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda amesema serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imetoa zaidi ya Tshs. Bilioni 40 kwa ajili ya kujenga na kukarabati miradi tisa ya umwagiliaji inayotarajia kuwanufaisha zaidi ya wakulima elfu 40 Mwanza na Geita .
Amebainisha hayo leo agosti 08, 2025 alipokua akihutubia maelfu ya wakulima, wafugaji, wavuvi na wajasiriamali katika kilele cha maadhimisho ya nane nane kanda ya ziwa magharibi yanayofanyika katika viwanja vya Nyamhongolo wilayani Ilemela.
Kadhalika ameeleza kuwa kwa kipindi cha 2020/25 serikali imetoa mbolea ya ruzuku ya Bilioni 6.4, Bilioni 4.7 kwa ajili ya ufugaji wa kisasa kwa vizimba ambapo zaidi ya vikundi 200 vimenufaika na Bilioni 263 zimetolewa kwa ajili ya chanjo za kuku na ng'ombe ndani ya mikoa hiyo.
Aidha, ameziagiza halmashauri kuendeleza viwanja hivyo kwa kuvijengea miundombinu ya kudumu na ya kisasa ili viwe na mazingira bora zaidi ya kuwahudumia wananchi katika kutoa elimu ya mashamba darasa kwa muda mrefu.
Akitoa taarifa ya maonesho hayo, Kaimu Katibu Tawala Msaidizi Uchumi na Uzalishaji Bw. Peter Kasele amesema wadau wameongezeka kutoka 1110 (2024) hadi 1234 (2025) ikiwa ni ishara ya wananchi kuhamasika kutaka kujua matumizi ya teknolojia katika kuongeza uzalishaji.
Aidha, ametaja changamoto ya kukosekana kwa miundombinu ya kudumu kwa ajili ya mashamba darasa na kusababisha gharama za mara kwa mara kwa kuweka miundombinu ya muda mfupi kila mwaka mathalani vipando, majosho, wajasiriamali, mabwawa ya uvuvi wa kisasa na maeneo ya unenepeshaji wa mifugo.
Ndugu Wenceslaus Venant ambaye ni mkulima kutoka Kisesa wilayani Ilemela aliyekopeshwa trekta la kisasa kwa ajili ya kilimo na benki ya Azania kwa kushirikiana na Agricom ameishukuru serikali kwa kujenga mazingira rafiki kwa taasisi za kifedha na kuweza kutoa mikopo kwa wakulima pamoja na wafugaji.
Kilele cha maonesho hayo kimechagizwa na utoaji tuzo na zawadi ambapo Aqwa Eagle (Magu) wameongoza katika uvuvi wa samaki, Fresrick Katundala (Nyamagana) ufugaji Nyuki, Mkulima bora akiwa ni ndugu Bulimi Zakaria (Kwimba) na Shija Mashauri (Nyang'hwale) akiibuka kidedea kwenye ufugaji bora wa ng'ombe wa nyama
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.