MIKOPO KWA WAFANYA BIASHARA WADOGO MWANZA IHARAKISHWE- WAZIRI GWAJIMA
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima ametaka zoezi la utoaji wa mikopo kwa wafanyabiashara wadogo mkoani Mwanza lifanyike haraka kwani tayari Serikali imetoa fedha Tshs. bilioni 5.
Akizungumza leo Februari 10, 2025 kwenye ukumbi wa Ofisi ya mkuu wa mkoa wa Mwanza na viongozi wa Shirikisho la wafanyabiashara hao SHIUMA katika mkutano wa dharura, Waziri Gwajima ametoa maelekezo kuanzia ngazi ya Wizara yake,Mkoa na Halmashauri kuhakikisha mchakato wa awali wa usajili na hatimaye kupata vitambulisho ili wapate mikopo hiyo ukamilike haraka.
Awali kiongozi huyo mwandamizi wa Serikali mara baada ya kusomewa taarifa za usajili za wafanyabiashara hao kwenye Halmashauri zote za Mkoa wa Mwanza alionesha kutoridhishwa na idadi ndogo huku kasi ya usajili ikienda kwa kusua sua.
"Hii hali siwezi kuikubali licha ya kikao hiki cha dharura,nimewasikia watenda wote nilichokibaini ni baadhi kushindwa kutekeleza majukumu yao na mwishowe ni kuwachonganisha wafanyabiashara hao na Mhe.Rais,hii siyo sawa," Waziri Gwajima.
Kuhusu Mwanza kutopata Ofisi ya Shirikisho la SHIUMA, licha ya fedha kuletwa mkoani humo mara baada ya Rais kuridhia kutoa fedha kwa mikoa yote ya Tanzania Bara, amewataka viongozi hao kuandika barua kwa kufuata taratibu zote na nakala apatiwe ili aweze kupata nafasi ya kuijengea hoja suala lao na siyo kufanya mawasiliano kwa njia ya simu pekee.
Afisa Maendeleo ya Jamii mkoani Mwanza Bi.Janeth Shishila ameomba Wizara ione namna ya kuwawezesha vifaa zikiwemo Kompyuta maafisa maendeleo ngazi ya kata ambapo mchakato huo wa usajili unaanzia huko.
"Hali ya kusua sua usajili wa wafanyabiashara wadogo imechangiwa na watendaji kukosa vitendea kazi vya msingi na hakuna kifungu kinachowapa fedha huko kwenye halmashauri," amesisitiza Bi.Janeth.
"Tunamshukuru Rais kwa nia yake njema kwetu sisi wafanyabiashara wadogo lakini wapo baadhi wanao fanya hujuma ili hizi fedha zishindwe kuwafikia walengwa na kunufaika wasiohusika." Msemaji wa Shirikisho la wafanyabiashara, Jumanne Ayoub.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.