RC MTANDA AAGIZA HOJA ZA KIMAKOSA KUMALIZWA HARAKA
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda ameitaka Halmashauri ya Jiji la Mwanza kuzimaliza na kuzifunga hoja za Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ambazo zimetokana na makosa madogo madogo kwa kurekebisha makosa yaliyofanyika ili kuzimaliza hoja hizo.
Mkuu wa Mkoa ameyasema hayo leo juni 17, 2025 wakati akizungumza katika Baraza la Madiwani kuhusu hoja za Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) katika Halmashauri ya Jiji la Mwanza na kuwataka Maafisa Manunuzi na Maafisa Sheria wa Halmashauri kufanya kazi kwa pamoja katika kuzimaliza hoja hizo zilizojitokeza kutokana na makosa.
“Kama jambo lilifanywa au lilikosewa hata kama na watu waliopita kwa bahati mbaya na kupelekea kuibuka kwa hoja, ushauri wangu mliopo ni lazima kuhakikisha mnakaa chini mnaomba maoni ya CAG ya kuona namna ya kufuta hoja hizo”. Amesema Mkuu wa Mkoa.
Endapo nitaendelea kuwa Mkuu wa Mkoa huu wa Mwanza nikija tena katika Baraza la namna hii na nikakautana na hoja za namna hizi kwa kweli hatutaoneana muhali. Amesisitiza Mkuu wa Mkoa.
Kuhusu hoja ya uwepo wa vyumba wazi katika Stendi ya Mabasi Nyegezi, Mkuu wa Mkoa ameitaka Menejimenti ya Jiji la Mwanza kuketi upya na kubadili mpango wa awali na kuja na mpango mpya unaoendana na uhalisia wa muktadha huo.
“Mimi nashauri ni bora kupata kidogo kuliko kukosa kabisa, kama vyumba vingine mlipanga kuweka hoteli na hamna mwekezaji aliyejitokeza msiendelee kusubiri badilisheni mpango” Ameongeza Mkuu wa Mkoa.
Halmashauri ya Jijij la Mwanza ilikuwa na Jumla ya Hoja 84, Kati ya hizo hoja za miaka ya nyuma zilikuwa 45 na hoja za mwaka wa fedha 2023/2024 zilikuwa 39. zilizofungwa baada ya uhakiki ni 35 hivyo hoja zilizobaki hadi sasa ni 49.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.