WACHEZAJI WA PAMBA JIJI FC WAOGA NOTI, RC MTANDA AWAPA SOMO WAAMUZI
Wachezaji wa timu ya soka ya Pamba Jiji FC wameoga noti shilingi milioni 15 na kuahidiwa nyongeza nyingine kama hiyo ndani ya siku chache kama muendelezo wa motisha huku Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda akiwakumbusha waamuzi kuzingatia sheria 17 za mchezo wa soka.
Katika hafla fupi ya kuwakabidhi fedha hizo iliyofanyika leo Februari 10,2025 kwenye uwanja wa michezo wa shule ya Sekondari Lake, RC Mtanda amebainisha kuwa soka ni mchezo wa burudani na amani lakini akitokea mwamuzi na tafsiri tofauti atasababisha jazba na vurugu.
"Rai yangu kwa waamuzi, sasa hivi ligi kuu ipo hatua ya lala salama waamuzi wadumishe amani michezoni kwa kuchezesha kwa haki dimbani, mashabiki wanapenda burudani na siyo vinginevyo”. amesisitiza Mhe. Mtanda ambaye pia ni mlezi wa timu ya Pamba Jiji.
Katika hafla hiyo Mkuu huyo wa Mkoa amefafanua kila ushindi kwa timu za uzito wa juu kama Simba, Yanga na Azam motisha itakuwa shilingi milioni 15 huku Ile walivyokubaliana na uongozi kwa timu nyingine ushindi motisha ni shs milioni 10.
"Nimeahidi kwa ushindi dhidi ya Azam tutawapa shs milioni 15 lakini kuna baadhi ya wadau wa soka wa Mkoa wetu wamefurahishwa na mwendo mzuri wa timu na kuniunga mkono kwa kunichangia fedha, sasa baada ya siku chache nitawakabidhi shs milioni 15 nyingine na kufanya jumla iwe milioni 30”. Mhe. Mtanda.
Mfungaji wa bao la ushindi mchezaji Deus Kaseke amekabidhiwa kitita cha sh. laki saba na nusu, mfungaji wa bao lililokataliwa Salehe Masoud ameondoka na kibunda cha laki mbili na nusu, mchezaji aliyetoa pasi iliyozaa bao la ushindi Yonta Camara amepata sh. laki moja pamoja na mlinda mlango Yona Amos amekabidhiwa laki moja kwa muendelezo wa kutoruhusu nyavu zake kutikiswa.
Aidha Mkuu huyo wa Mkoa amewaomba wale wadau wenye nia njema na Pamba Jiji walete michango yao kupitia Ofisi ya Mkuu wa Mkoa au Mkurugenzi wa Jiji ili kuzidi kuwapa motisha wachezaji wa timu hiyo ambayo Jumamosi hii watawakaribisha Coastal Union kwenye uwanja wa CCM Kirumba.
Pamba Jiji FC maarufu kama TP Lindanda Wana Kawekamo baada ya ushindi dhidi ya Azam FC imechumpa hadi nafasi ya 12 na mtaji wa pointing 18 kibindoni katika msimamo wa ligi kuu.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.